


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda leo ametegua kitendawili kilichowatesa kwa muda mrefu wakazi wa Kata ya Liwiti baada ya mmoja wa wananchi kudai ndiye mmiliki halali wa eneo la soko lao jambo lililotaka kupelekea uvunjifu wa amani.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi hao Makonda ameagiza eneo hilo kurejeshwa kwa wananchi kwaajili ya matumizi ya soko baada ya kubainika kuwa anayedai eneo hilo aliuziwa kihalali alijichanganya badala ya kwenda kiwanja kilichopo Block No. 200 A kujikuta anakwenda Block No. 200B ambacho kwa mujibu wa Ramani ya Mipango miji ni eneo la umma.
Kutokana na Mkanganyiko huo Makonda ameagiza mama huyo kuonyeshwa kiwanja chake cha Block No. 200 A na kuagiza asitokee mtu yoyote wa kuwabugudhi wananchi na eneo lao la soko.
Aidha Makonda ameagiza kuvunjwa mara moja ukuta wa mwananchi aliyejenga kwenye eneo la hifadhi ya barabara na kusababisha usumbufu kwa wakazi wa mtaa wa amani kata ya Tabata Liwiti kukosa sehemu ya kupita na kujikuta wanazunguka umbali mrefu.
Makonda pia ameagiza Uwanja wa mpira wa Tabata Sigara kurejeshwa kwa wananchi kwaajili ya matumizi ya michezo baada ya wananchi kulalamika kuwa aliyenunua magorofa ya Sigara anadai kuwa amenunua pia eneo la kiwanja na kusababisha kukosekana kwa eneo la michezo.
Sambamba na hayo Makonda amempongeza Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bona Kalua kwa kuendelea kuwasemea wananchi juu ya kero zinazowasumbua hadi kuzifikisha ofisini kwa mkuu wa mkoa.
Kwa upande wao wakazi wa Kata ya Liwiti wamefurahia kuona migogoro yao ya muda mrefu imetatuliwa kwa mpigo ambapo wamempongeza Makonda kwa usimamizi mzuri wa sheria huku wakimpongeza Rais Magufuli kwa kuwateua Makonda anayewatatulia shida zao.