×

Kizungumkuti: Muna Awasili Airport Bila Mwili wa Patrick – Video

 

TAARIFA zilizotufikia zinaeleza kuwa, Msanii wa Bongo Movie, Rose Alphonce maarufu kama ‘Muna Love’ amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam bila mwili wa marehemu mtoto wake, Patrick tofauti na matarajio ya waombolezaji waliofika wakiwa na matumaini ya kupokea mwili huo.

 

Muna amewasili kwa ndege leo Julai 6, 2018, majira ya saa 7 mchana akitokea Nairobi nchini Kenya alikokuwa akimuuguza mwanaye kabla ya kukutwa na mauti. Dakika chache baada ya kuwasili, msanii huyo alianguka na kupoteza fahamu ambapo alichukuliwa kwenye gari na kuondoka uwanjani hapo.

 

Taarifa zinaeleza kuwa, mwili wa mtoto patrick huyo uliwasili hapa nchini kimya kimya jana usiku na kupelekwa Mbezi, huku ikidaiwa kuwa huenda lengo lake ni kama alivyoeleza awali kwamba anataka yeye ndiyo asimamie msiba wa mwanaye na kumzika na si baba yake Peter Zacharia ambaye jana ilisemekana wameelewana na Muna kuhusu taratibu za msiba na mazishi.

 

Wengine wanadai mwili umewasili na kuchukuliwa kabla ya waombolezaji na wanahabari hawajafika huku taarifa nyingine zikidai mwili utafika na ndege ya saa 11 jioni na taarifa nyingine zikieleza kwamba baada ya kuishiwa nguvu na kuanguka, Muna aliondoka na nyaraka muhimu za mwili wa marehemu hivyo ikashindikana kutolewa. Global Publishers inaendelea kufuatilia na tutakujuza kila kitakachojiri.

Awali, ilielezwa kwamba mwili huo ungewasili leo majira ya saa 5 asubuhi na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo kesho ungeagwa katika Viwanja vya Leaders na kuzikwa katika Makaburi ya Kinondoni.

Kwa taarifa ya mwandishi wa www. globalpublishers.co.tz aliyeko Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere amesema kwa sasa waombolezaji na wanahabari wote wameondoka na kuelekea Mbezi ambako mwili ulipelekwa jana baada ya kuwasili.

 

(PICHA: RICHARD BUKOS | GPL)

Breaking News: Muna Awasili Airport Bila Mwili wa Patrick – Video