×

NMB YAPATA TUZO BORA  KUTOKA EUROMONEY NCHINI UINGEREZA

Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker, (kushoto) akishikilia tuzo  kutokana na Benki ya NMB kuwa  yenye faida zaidi nchini Tanzania.

 

 

JARIDA kongwe nchini Uingereza linalojihusisha na masuala ya utafiti wa kiuchumi na kibiashara la Euromoney, limeitangaza Benki ya NMB, kuwa Benki Bora ya Mwaka nchini Tanzania, ikiwa ni mwaka wa sita mfululizo.

 

 

 

Tuzo hiyo iliyotolewa juzi jijini London, inaifanya NMB kuwa Benki yenye faida zaidi Tanzania, inayotokana na uimara wa taasisi hiyo katika Sekta ya fedha, iliyofanya vyema kupitia mabadiliko ya kimfumo yanayohusisha huduma za kidijitali.

 

 

Ikizungumzia mafanikio hayo, Euromoney katika taarifa yake imesema NMB kuwa Benki Bora Tanzania, kumezingatiwa vitu vingi, ikiwemo utoaji elimu za kifedha, mabadiliko ya kimfumo katika fedha na kutanua fursa za jamii kutumia huduma za kifedha.

 

 

Taarifa hiyo iliongeza kuwa uwekezaji wa NMB katika teknolojia, umeleta ufumbuzi wa changamoto za kushughulikia mahitaji ya wateja kwa njia za kimtandao (mobile banking), kadi za benki na mawakala wanaotoa huduma.

 

 

Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker, amesema benki yake inajisikia fahari na kujivunia ushindi wa kihistoria waliouweka kwa kuibuka washindi wa tuzo hiyo kwa miaka sita mfululizo.

 

 

Alibainisha ya kwamba, wanapenda kutumia fursa hiyo kuwashukuru wateja wao, ambao ndiyo wanaowasukuma katika kuwabunia huduma bora na kwamba wanaichukua tuzo hiyo kama chachu ya kuendelea kutanua huduma bora kwa jamii.

 

 

Bussemaker alisisitiza kuwa, benki yake inajivunia uanzilishi wa mabadiliko ya kimfumo kwenda dijitali, ambayo ni sehemu ya mchakato wao wa huduma bora kwa wateja na kwamba tuzo hiyo ni matunda ya safari ya ushirikiano baina ya benki na wateja wao.