×

SIMBA WALIVYOELEKEA UTURUKI ALFAJIRI YA LEO

KIKOSI  cha Simba chenye jeuri ya noti za mwekezaji Mohammed Dewji ‘MO’ leo  kimeondoka  kuelekea kwenye ardhi ya Antalya ambayo timu kibao za kishua duniani zimepiga kambi.

 

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Simba kuweka kambi hapo katika miaka ya hivi karibuni kwani walikuwa wakijichimbia Afrika na Arabuni. Msafara wa wachezaji 26 wa Simba umeondoka leo Jumapili saa 10 alfajiri tayari kwa kambi ya wiki mbili na watarejea nchini Agosti 5. Wachezaji Mwinyi Kazimoto, Moses Kitandu, Jamal Mwambeleko, Ally Shomary na Said Mohammed hawakusafiri kutokana na sababu mbalimbali.

Simba ambayo itacheza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika Novemba 27, itakutana na timu zingine zaidi ya 50 kutoka katika nchi mbalimbali duniani zitakazopiga kambi mjini Antalya, Uturuki kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Utalii wa Michezo wa nchini humo.

Mwenyekiti wa Umoja wa Utalii wa Michezo wa Uturuki, Recep Yasacan amesema mji huo ambao saa zake zinakwenda sawa na Tanzania, una viwanja 157, vilivyopitishwa na wataalam wa Fifa na watapokea ugeni wa timu 1500 mwaka huu.

 

Spoti Xtra linajua kwamba Saudi Arabia, Kuwait na Libya ni miongoni mwa timu hizo na kwenye wiki ya pili ya mazoezi ya Simba itacheza nazo mechi tatu za kirafiki ambazo zitakuwa zimepangiliwa na mratibu wa kambi ya Simba nchini huo. “Utalii wa michezo unaitambulisha Uturuki duniani, nchi zote za Ulaya zimefanya mazoezi hapa,”alisema Recep akiizungumzia sehemu hiyo ambayo Yanga imewahi kuweka kambi kipindi cha nyuma ikiwa chini ya bilionea Yusuf Manji.

Klabu zote za Ligi Kuu ya Azerbaijan pamoja na Urusi na Uturuki zimeweka kambi Antalya. Nyingine ni kutoka Urusi huku kadhaa zikiwa zinakamilisha mchakato wa kuingia nchini humo kama Simba.

 

Antalya ni eneo maarufu duniani ambalo timu mbalimbali hupenda kuweka kambi kutokana na utulivu wake pamoja na vifaa mbalimbali vya kisasa ikiwemo viwanja vizuri na vyenye kila huduma ambayo inahitajika na wanamichezo.

Hoteli zote kwenye mji huo uliozungukwa na fukwe zenye kila aina ya starehe, zina viwanja vyake vya michezo mbalimbali ambapo timu ina uwezo wa kufanya mazoezi muda wowote kulingana na ratiba yao.

 

Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma ameliambia Spoti Xtra kwamba kambi hiyo wataitumia kikamilifu na itawasaidia kuwajenga wachezaji kisaikolojia na kumpa nafasi kocha mpya Patrick Aussems kuwajua.

 

Djuma alisema kuwa kambi hiyo itawaimarisha kwani wakirudi Dar es Salaam watakuwa moto wa kuotea mbali kwenye Ligi Kuu Bara inayoanza Agosti 22, Simba ikipangwa kuanza na Prisons jiijini Dar es Salaam.

Habari za ndani zinasema kwamba nauli ya kila mchezaji kwenda Uturuki ni Sh.Milioni 2.2 na idadi kubwa ya watalii wamekuwa wakimiminika kwenye mji wa Antalya kupumzika. Hiyo inamaanisha kwamba watu 26 walioondoka wameigharimu Simba zaidi ya Sh.Milioni 58 ambazo kwa hali ngumu ya uchumi iliyoko kwa watani zao wa jadi Yanga ingeweza kutosha kuwasajilia wachezaji wawili au watatu wazawa.

 

Simba wanainjoi maisha kwa sasa kutokana na mizuka ya MO ambaye anataka kikosi hicho kitishe msimu ujao na kufanya vizuri hususani kwenye michuano ya kimataifa