
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, imempatia kibali cha kufanya kazi nchini Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye ataanza kukaa kwenye benchi katika mchezo dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.
Kocha huyo alitua nchini Aprili 23, mwaka huu akichukua nafasi ya Mzambia, George Lwandamina ambaye tangu amekuja nchini hakuwahi kukaa kwenye benchi la timu hiyo.
Kocha huyo Mkongo aliikosa michezo kadhaa ya Ligi Kuu Bara na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika wanayoshiriki hivi sasa na Jumapili hii watacheza na Gor Mahia ya Kenya kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Zahera amesema kwa mara ya kwanza anatarajia kukaa katika benchi kwenye mchezo ujao dhidi ya Gor Mahia.
“Ninafuraha kubwa kupatiwa kibali cha kufanyia kazi hapa nchini baada ya muda mrefu viongozi kuniangaikia kibali hicho.
“Kibali hicho kimepatikana jana (juzi) baada ya viongozi kunipa taarifa za kupatikana kibali hicho, Jumapili hii nitakuwepo kwenye benchi nikiiongoza Yanga,” alisema Zahera.
Aidha, Meneja Mkuu wa Yanga, Hafidh Saleh alithibitisha kupatikana kwa kibali cha kufanyia kazi na ITC ya mshambuliaji mpya Mkongoman, Heritier Makambo.
“Pia, jana (juzi) tulitumiwa leseni za Kaseke (Deus) na Matheo (Anthony) kutoka Caf zikiwaruhusu kucheza mechi dhidi ya Gor Mahia, hivyo watakuwepo kwenye sehemu ya kikosi chetu tutakachokitumia siku hiyo,” alisema Saleh.
Na Wilbert Molandi, Championi Ijumaa