
RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, jana (Jumapili) mapema asubuhi alifika nyumbani kwa Mkurugenzi wa Makampuni ya Global Group, Eric Shigongo, Mikocheni jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kumpa pole kwa kuondokewa na mama yake mzazi Bi. Asteria Kahabi Kapela aliyefariki Julai 27 mwaka huu.

Rais huyo alifika nyumbani hapo na kutoa heshima zake za mwisho huku akimpa maneno ya faraja mkurugenzi huyo, kwenye kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mama yake.

Akitoa shukrani zake kwa rais, Shigongo alimshukuru kiongozi huyo wa nchi kwa moyo aliouonyesha pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kufika kumfariji. “ Namshukuru kila mmoja aliyeacha shughuli zake na kuja kujumuika na sisi maana kila tunapowaona tunazidi kufarijika kuliko tungekuwa peke yetu.

“Ujio wa rais ni wa kipekee, mimi na familia yangu tumefurahi, tumetiwa ujasiri wa kupokea msiba huu kwa mapenzi ya Mungu. “Lakini sitaacha kumshukuru kiongozi na ndugu yangu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa na viongozi wengine wa kada zote, ndugu na jamaa, majirani na kila aliyegushwa na msiba huu, nimetambua kuwa ninao ndugu wengi wanaonipenda.
“Sina cha kumlipa kila mtu zaidi ya kuwaombea kwa Mungu baraka na neema tele, nawaomba tuzidi kuombeana ili shughuli zote za msiba huu ziweze kukamilika salama,” alisema Shigongo alipozungumza na gazeti hili.
Hadi gazeti hili linakwenda mtamboni mwili wa mama wa mkurugenzi huyo, Bi Asteria, ulikuwa ukiandaliwa kwa safari ya kuelekea nyumbani kwa marehemu Nyakato Mecco, Mwanza.
Aidha baada ya kumaliza shughuli zote mkoani Mwanza mwili huo utasafirishwa tena kwenda katika kijiji alichotoka marehemu cha Bupandwamhela, Buchosa wilayani Sengerema mkoani Geita kupumzishwa katika nyumba yake ya milele siku ya Jumatano Agost 1,2018. Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiweAMINA