MOROGORO: Moro kunani? Siku chache baada ya kutokea kwa tukio la paka kumng’ata bibi maeneo ya Mwembesongo, mwanzoni mwa wiki hii nyoka mkubwa mwenye rangi ya dhahabu amezua kizaazaa baada ya kuibuka katikati ya Mji wa Morogoro na kuzua tafrani ya aina yake hali iliyosababisha shughuli zisimame kwa muda.
Tukio hilo lilitokea eneo la Lunna kwenye makutano ya barabara za Madaraka, Makongoro na Uhuru, eneo ambalo baadhi ya machinga wamepanga biashara zao kandokando ya barabara hizo.
Wakati nyoka huyo aliopoonekana, umati mkubwa wa watu ulikusanyika eneo hilo na kusababisha foleni kubwa ya magari, pikipiki, baiskeli na watu wanaotembea kwa miguu.
Amani lilipofika eneo la tukio na kushuhudia umati mkubwa, lilielezwa kuwa nyoka huyo alionekana kwenye banda la nguo la mmachinga aliyefahamika kwa jina la Fredi Adrew.
Akizungumza na Amani Adrew alisema tukio hilo limetokea alfajiri wakati alipokuwa akifungua eneo lake la kazi ndipo alipopiga kelele na watu wakajaa.
“Yaani ni bahati ya Mungu tu, asubuhi wakati nafungua ofisi yangu ghafla nimeliona hili joka la ajabu lenye rangi ya dhahabu likirandaranda ndani ya banda langu.
“Kama unavyoona hapa ni katikati ya mji hakuna majani wala majengo mabovu huyu nyoka ametoka wapi? Au ametumwa na wapinzani wangu wa kibiashara najiuliza kwa nini iwe kwangu?
“Mabanda hapa kwetu yako mengi hapa na langu liko katikati kwa nini aje kwangu tu? Ila mimi namuamini Mungu tu,” alisema machinga huyo huku akionekana kujawa na hofu kubwa.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alienda mbele zaidi kwa kuhusisha na masuala ya kishirikina mambo ambayo yalionekana kupingwa na baadhi ya mashuhuda wengine.
“Mh! Nyoka wa rangi hii akionekana mjini kama hivi ni wa kutumwa tu,” alisikika shuhuda mmoja ambaye hakupenda kutaja jina lake.
Hata hivyo mashuhuda wengine waliozungumza na Amani kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema tukio hilo ni la kawaida kwani nyoka anaweza kukaa popote kwa kutegemea na mazingira yaliyopo.
“Huwezi kujua jirani hapa kunaweza kuwa na mitaro na nyoka akajibanza halafu usiku akatoka labda ndo akaja hapa kwenye biashara za wamachinga,” alisikika mmoja wa mashuhuda.
Hata hivyo, wananchi waliokuwa wamezingira eneo hilo walimuua nyoka huyo kisha wakamchoma moto.
Agosti 15, mwaka huu gazeti la Risasi Mchanganyiko liliripoti tukio lingine la ajabu lililozua taharuki baada ya paka kumtokea Khadija Ramadhan (67), mkazi wa Mtaa wa Mwigole, Kata ya Mwembesongo mkoani Morogoro, kumzunguka kisha kumng’ata mguuni.
Stori: Dunstan Shekidele, Amani