
SIKU hizi ukisikia mtu anasema ‘Dunia simama nishuke,’ inamaanisha mambo ya duniani yamemchosha; na kweli unyama unaofanyika hivi sasa katika jamii unaonesha kwamba tumefika pabaya. Mume kumtesa mkewe wa ndoa kwa zaidi ya saa 4, kisha kumchinja na kumkatatakata kwa panga sehemu mbalimbali za mwili, ni tukio la ukatili wa aina yake, lakini Nyakwanga Makongoro (48) anadaiwa kulifanya, bila mwili kumsisimka.
Nyakwanga mtuhumiwa anaishi Kijiji cha Kiroreli Kitongoji cha Msiriganyi, Kata ya Nyamuswa wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Uwazi limeambia kuwa mke aliyechinjwa kikatili anaitwa Sousoni Chamriho ‘24’ (pichani). Hakufa tu lakini maiti yake iliyotapakaa damu ililazwa kitandani usiku kucha sambamba na watoto wake watatu aliowaacha yatima.
Usiku wa manane Agosti 16 mwaka huu, ndiyo ilikuwa siku ya Sousoni kuiaga dunia kwa kuuawa, huku madai yakiwa ni usaliti wa kimapenzi. Kisa cha Nabii Issa Bin Mariamu au Yesu kinaeleza kuwepo kwa watu waliompelekea mwanamke mzinifu na kuomba ridhaa yake wampiga mawe hadi afe lakini Nabii aliwajibu hivi:
“Asiyekuwa na makosa awe wa kwanza kumpiga mawe.” Maandiko yanaeleza kuwa wote waliokuwa wamekusanyika walitawanyika kuonesha kuwa kila mmoja alihukumiwa kukosa katika nafsi yake. Kwa vyovyote ilivyo; Sousoni awe alisaliti ndoa yake au la hukumu ya kifo haikumstahili kwa sababu hata mtuhumiwa alikuwa na makosa yake, ilifaa kusamehena.
TULIANGALIE KISA NA TUKIO LENYEWE
Inaelezwa na chanzo cha habari kuwa mtuhumiwa wa mauaji siku ya tukio alirudi mapema majira ya saa mbili usiku na kumkuta mkewe akiwa na watoto wao watatu nyumbani wakiendelea na yaliyokuwepo. Baada ya salamu zisizokuwa na bashasha, Nyakwanga alianza kumuuliza mkewe kwa nini anasaliti ndoa?
Pengine swali hilo lilikuwa na mshangao kwa mkewe lakini kwa sababu lilitaka maelezo alimwambia mumewe kuwa hana mwanaume yeyote anayetembea naye pale kijijini.
Nyakwanga kama mtu aliyekuwa na lake jambo kwa muda mrefu alimtajia mkewe jina la mwanaume aitwaye Sumuni na kutaka kupata maelezo kuhusu uhusiano wao. Pamoja na mkewe kukataa katakata kujivinjari na Sumuni lakini mume aliendelea kung’ang’ania anachokiamini huku akimtaka mkewe akiri bila kushurutishwa sana.
WAENDA SERIKALINI USIKU
Baada ya mke kuendelea kugomea usaliti Nyakwanga aliamua waende kwa mwenyekiti wa kitongoji mahali ambapo aliamini kuwa mkewe angekiri kosa la usaliti.
Chanzo kinasema Saa 3: 26 usiku mume na mke walifika kwa mwenyekiti wa kitongoji kuomba suluhu lakini mwenyekiti aliwataka waende wakalale na kwamba shauri lao lingesikilizwa asubuhi. Lilikuwa kosa la fisi kukabidhiwa bucha, Nyakwanga aliporudi nyumbani akiwa na mkewe aliendeleza ‘wimbo wa Sumuni’ ikawa; Sumuni, Sumuniiii, mara akaanza kumpiga mkewe.
Mayowe ya ‘nakufa, nakufaa jamani’ yalisikika kwa majirani; wachache waliamka kwa lengo la kwenda kumsaidia mwanamke huyo, lakini kwa sababu Nyakwanga anadaiwa kuwa na misuli minene wote walimgwaya.
“Tunamugopa kweli kwa sababu ni mkorofi halafu ana nguvu, alipotutishia kuwa atatukatakata mapanga tukaondoka na kuwaacha wakiendelea kugombana na mkewe,” jirani wa Nyakwanga ambaye hakupenda jina lake liandikwe aliliambia Uwazi.
USIKU WA MANANE KUKAWA KIMYA
Baada ya kuwepo kwa zogo kubwa kwa muda mrefu zaidi ya saa 3 ulipofika usiku wa manane hali ya ukimya nyumbani kwa Nyakwanga ilitawala.
Walichoamini majirani ni kwamba shetani alikuwa ameepukwa na kwamba yote yamepita, kumbe haikuwa hivyo; mwanamke huyo alikuwa amechinjwa tayari na kurudi alikotokea. Kama kuchinja na kuua hakukua na maana, mtuhumiwa aliamua kuchukua panga lenye makali ya kutosha na kuanza kuuchanga mwili wa marehemu sehemu mbalimbali.
Damu kama mto zilitapaa chumbani, Uwazi lilifanikiwa kuziona lakini maelezo ya kuumiza zaidi ni pale ilipodaiwa kuwa baada ya kufanyika kwa unyama huyo mtuhumiwa aliwachukua watoto wake waliokuwa wakishuhudia uuaji ule na kuwaketisha chini; akawaonya wasipige kelele. Masikitiko zaidi watoto wenyewe mmoja ana umri wa miaka 6, mwingine 4 na wa mwisho 2, ambao majina yao yanahifadhiwa kulinda maadili.
ASUBUHI YA HUZUNI
Siku iliyofuata majira ya saa 2 asubuhi kaka wa mwanamke huyo aitwaye Mugusi anadaiwa kumpitia dada yake waende gulioni kuuza pamba, lakini alipofika nyumbani kwa Nyawanga alipisha hodi isiyokuwa na majibu.
“Nikaamua kusukuma mlango, nilipoingia nikakuta damu nyingi chumbani halafu kitandani kuna watu wamelala huku wamefunikwa shuka, nilipoifunua nikakuta dada yangu ameuawa huku watoto wake nao wakiwa wamelazwa pembeni huku wakiwa wamelala fofofo na mdomoni wametapakaa damu,” alisema Mugusi.
Mugusi alipoona hali hiyo akawaita majirani ambao walifika na kushuhudia mauwaji hayo ya kutisha lakini kilichowaliza wengi ni pale walipowaona watoto wa marehemu wakiwa wamelowa damu.
MTOTO ASIMULIA MAMA YAKE ALIVYOUAWA
“Alimpiga mama kwa muda mrefu, sisi tukawa tunaogopa tu, baadaye tukaona anachukua panga akatulaza chini akamuua mama. “Tulipotaka kupiga kelele akatufokea,” alisema mtoto wa kwanza wa marehemu.
Alipouliza kuhusu kutapakaa damu hadi midomini alisema baba yao aliwaza kitandani kwenye damu nyingi za mama yao ambapo madai ya kunyweshwa damu ya marehemu yalipotolewa mayowe hasa ya wanawake yalisikika eneo la tukio.
RPC HUYU HAPA
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Juma Ndaki amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo ya kinyama na akasema mtuhumiwa huyo alitoroka muda mfupi baada ya kutenda unyama huo mbele ya watoto wao.
Kamanda Ndaki akasema : “Tumemkamata mtu mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Sumuni ambaye ndiye aliyekuwa akilalamikiwa na mtuhumiwa Nakwanga kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe na kuwa yeye ndiye chanzo cha mauaji hayo ambapo uchunguzi unaendelea.”
Mtuhumiwa ambaye picha yake ndogo imetumika kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti hili bado anayendelea kusakwa kwa mauaji baada ya kutoroka.
NENO LA UWAZI
Uwazi linalaani vikali mauaji haya na kuishauri jamii na hasa wanandoa kuacha tabia ya kulimbikisha truhuma bila kuzitatua kwani kufanya hivyo kunaleta msongo mkubwa wa mawazo ambao mwisho wa siku husababisha matukio mabaya yakiwemo ya kuua au kujiua.
Inashauriliwa kwamba kila palipo na hali ya kutoelewana ni vyema kuketi na kuzungumza ikiwepo kuombana msamaha na pale suluhu ya wawili inapokosekana basi atafutwe mtu wa tatu lengo likiwa ni kutafuta muafaka.
Stori: GREGORY NYANKAIRA, Mara