WAMILIKI wa vyombo vya usafiri Hiace maarufu kama daladala katika manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma leo wamesitisha huduma ya usafirishaji wa abiria wakiishinikiza serikali kusikiliza madai yao ya kuviondoa vyombo vya usafiri wa bajaji na magari madogo maarufu kama michomoko ambavyo wamedai vinafanya kazi bila kuzingatia sheria zilizopo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wamiliki wa Mabasi Mkoa wa Kigoma (KIBOA), Almasi Juma amesema maamuzi hayo yametokana na kutosikilizwa kwa madai yao tangu mwaka 2014 na hivyo kulazimika kusitisha huduma kwa muda usiojulikana hadi hapo serikali itakapokubali kutatua mgogoro wao.
Baadhi ya wananchi wameeleza adhari zilizojitokeza kuwa ni pamoja na kushindwa kufika maeneo yao ya kazi lakini pia wanafunzi kushindwa kufika shule kwa wakati.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga ametoa wito kwa vyombo vingine vya usafirishaji kuomba vibali na kuanza kazi ya usafirishaji wa abiria huku akiwataka wamiliki waliogoma kufika ofisini kwake ndani ya saa 24 na atakayekiuka hatua kali zitachukuliwa ikiwemo kufutiwa leseni zao.