



WATUMISHI wa Mahakama ya Tanzania wamekumbushwa kuendeleza na kuthamini maboresho yanayoendelea ndani ya Mahakama kupitia Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama.
Hayo yalisemwa jana na Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma Mh. Ignas Kitusi jijini Dodoma alipokuwa akifunga rasmi mafunzo ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu za ndani za Mahakama yaliyohusu usimamizi na udhibiti wa fedha za miradi ya wafadhili.
“Kila mmoja ana jukumu kwenye mradi huu wa maboresho unaofadhiliwa na Benki ya Dunia. Hivyo tunawajibika kuhakikisha tunasaidia mradi huu katika kuongeza tija kwa Mahakama” Alisisitiza Mhe. Jaji Kitusi .
Katika hotuba yake kwa washiriki wa mafunzo hayo, Mhe. Jaji Kitusi aliwasihi Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu za Mahakama kushauri namna bora katika kuwezesha kuongezeka kutumika kwa fedha za mradi.
Mhe. Kitusi alisema kupitia mafunzo hayo ana uhakika yatasaidia kuongeza uwezo na vilevile amewashauri Wahasibu hao kuwa wawezeshaji wa pesa kutumika badala ya kuwa kikwazo.
“Hivyo mna kazi kubwa ya kushauri namna bora katika kutumia ,siyo kuzuia tu pesa isitumike bila sababu za msingi,” alisema Mhe. Jaji Kitusi
Nao washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Mahakama ya Tanzania, Benki ya Dunia na Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto kwa kufanikisha mafunzo hayo ambayo yamewaongezea maarifa, ujasiri na uelewa mpana katika manunuzi na namna bora ya usimamizi na udhibiti wa fedha za mradi wa maboresho ya Mahakama.
Na Rashid Omar, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Pwani.