



WAVUVI wanaofanya shughuli zao katika eneo wa Kunduchi jijini Dar es Salaam, wameiomba Manispaa ya Kinondoni kuwaruhusu kwenda kufanyia biashara zao za kuuza samaki katika soko la Feri kwani eneo lao hapana wanunuzi na wanakuwa na samaki wengi.
Hayo waliyasema wakati walipokuwa wakizungumza na Mkurugenzi wa Kampuni ya Laxspacer International Ltd, Kasmiry Mwabena, ambao ni wakusanyaji wa kodi za serikali ambapo aliwataka wavuvi hao kuchukua risiti pale wanapokuwa wamelipia kodi ili kurahisisha kutodaiwa tena wanapohitaji kwenda wilaya nyingine kuuza samaki hasa soko la Feri la Wilaya ya Ilala kwani lipo ndani ya mkoa mmoja.
Mwabena alisema kwamba tayari kuna baadhi ya viongozi wa upande wa wavuvi ambao wamekwenda kwa mkurugenzi wa wilaya ya Kindondoni na wamepanga kuangalia namna ya wavuvi hao watakavyoweza kutoa samaki sehemu moja kwenda nyingine kadiri watakavyoona.