×

SKENDO ZA WEMA , MAFANIKIO YA JOKATE MWEGELO

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo

MASHINDANO ya Miss Tanzania yamerejea kwa kishindo cha aina yake. Walimbwende takriban 20 wanatarajiwa kupanda jukwaani Septeba 8, 2018 ndani ya Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), Posta jijini Dar kuchuana ili mwishowe apatikane mkali kuliko wote ambaye atatuwakilisha katika mashindano ya dunia.

Nichukue fursa hii kwanza kuwapongeza waandaaji ambao ni Kampuni ya The Look Company Limited chini ya Mkurugenzi, Basilla Mwanukuzi (Miss Tanzania 1993). Nimefuatilia mchakato wa kuwapata wawakilishi kutoka kanda mbalimbali, sikusikia malalamiko yoyote na hata warembo waliopatikana kutoka mikoa mbalimbali wana vigezo, vijana wa mjini wanasema wote ni visu.

Kwa maana hiyo majaji katika fainali ya mashindano hayo watakuwa na kazi nzito ya kumchomoa moja ambaye atakuwa ni zaidi ya yote na niseme tu kwamba, endapo haki itatendeka, mrembo atayevalishwa Taji la Miss Tanzania 2018 ataleta ushindani mkubwa Miss World.

Lakini wakati tukielekea kwenye fainali hizo, kuna jambo moja ambalo nimelibaini kwa warembo wetu hawa mwaka huu. Alhamisi iliyopita, walitembelea Kampuni ya Global Publishers, wachapishaji wa Magazeti ya Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Uwazi, Risasi, Amani, Championi na Spoti Xtra. Wakiwa kwenye chumba cha habari cha Magazeti Pendwa, nilibahatika kubadilishana nao mawazo na nikagundua kuwa, wanaogopa sana skendo!

Niligundua hivyo baada ya kuwauliza kwamba, najua wote wanalitamani taji hilo na nikawakumbusha kuwa, mmoja wa warembo waliowahi kulitwaa ambaye mpaka leo ni staa mkubwa, ni Wema Isaac Sepetu, Miss Tanzania 2006/07. Nikawauliza kwamba ni nani kati yao angependa kufuata nyayo za staa huyo?

Cha ajabu alinyoosha kidole mrembo mmoja tu, waliobaki waliinamisha vichwa. Nikawauliza kwa nini hawataki kufuata nyayo za staa huyo, wote wakabaki kimyaa! Mmoja akaniliza; ‘unamaanisha kufuata nyayo za Wema kimafanikio au kiskendo?’ Baada ya mrembo huyo kuuliza swali hilo, baadhi ya warembo wengine walitikisa vichwa kuashiria kuwa, wanaungana na mwenzao kutaka kujua mamtiki hasa ya swali hilo.

Katika kulijibu, niliwaeleza kwamba, ukitaka kufuata nyayo za mtu, hutakiwi kubagua baadhi ya mapito yake. Wakati nikiendelea kufafanua, mmoja wa warembo hao akasema: “Unajua unaposema kufuata nyazo za mtu, Wema amekuwa na skendo nyingi.

Mimi: Kwa mfano skendo gani?

Mrembo: Za kubadili wanaume.

Mimi: Kwani kubadili wanaume ni skendo? Hivi yupo kati yenu ambaye tangu ameingia kwenye uhusiano amekuwa na mpenzi mmoja mpaka leo?

Wote: Hakuna!

Mimi: Kinachomponza Wema ni ustaa wake na kwamba anaingia kwenye uhusiano na wapenzi mastaa na kwamba akiwa na mtu hawezi kuficha na hata akiacha au kuachwa, haiwezi kubaki siri kwa kuwa ni staa na anafuatiliwa sana. Jitahidini kuiacha ‘nature’ ichukue mkondo wake.

Baada ya kuwafafanulia kidogo kuhusu skendo ya Wema ya kubadili wanaume, nikawauliza tena kwamba, ni nani kati yao angependa kufuata nyayo za Jokate Mwegelo ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe? Karibia nusu ya warembo hao walinyoosha mikono, baadhi wakabaki kama wanaotaka kunyoosha, lakini mikono yao ikawa mizito.

Hapo nikapata fundisho kubwa sana, kwamba, watu wengi huwa hawakumbuki ulikopita bali uko wapi kwa sasa. Ndiyo maana wengi walitamani kufuata nyayo za Jokate kwa sababu ametokea kwenye urembo na sasa ni mheshimiwa. Lakini warembo hao wanasahau kuwa, hata Jokate katika mapito yake, aliwahi kukumbwa na skendo ikiwemo ya kubadili wanaume.

Kwa hiyo ushauri wangu kwao ni kwamba, ukishakuwa Miss Tanzania, wewe ni staa! Na siku zote staa ni mtu ambaye watu wengi watakuwa wanataka kujua maisha yake yakoje? Amefanya kipi kizuri na kibaya? Kwa hiyo kikubwa ni kuwa ‘smart’ tu na kujitahidi kuwa makini katika kila hatua unayopita.

AMRAN KAIMA