MAMA anayeishi na familia yake na kufanikiwa kuzaa watoto wanne kufikia hatua ya kulala kando ya barabara si kitu cha kawaida, lakini Irene Samweli (31) mkazi wa Majimatitu, Mbagala jijini Dar es Salaam, yamemfika mazito.
Kwa macho mama huyo haonekani kuwa na matatizo ya akili wala kuwepo kwenye kundi la ombaomba wanaolala ovyo kwenye mitaa ya jiji lakini mwenyewe analieleza Risasi Jumamosi kilichomsibu hadi kufikia hatua hiyo.
“Nilikuwa naishi na mume wangu kwa upendo lakini kutokana na matatizo katika ndoa nimeshindwa.
“Nimeamua kuchukua watoto wangu na kuondoka naona amani kuishi au kulala mitaani na kando ya nyumba za watu kuliko kuishi kwangu.
“Si kwamba siumii naumia sana, kwanza hawa watoto wangu wawili walikuwa wanasoma imelazimika wakatize masomo.
“Maisha yamekuwa machungu kwangu na kwa wanangu, sina msaada, kwa sababu katika maisha haya utampelekea nani mzigo huu mkubwa wa watoto wanne aulee.
“Hapa unapotuona sehemu ya kulala shida, chakula hatuna, vifaa vya kujihifadhi nyakati za usiku hatuna tunalala kama wanyama.
AELEZA WATOTO WANAVYONUSURIKA KUBAKWA
“Kuna mitaa mingine usiku kuna vibaka wengi, wakati mwingine huwa wanakuja na kutaka kuwabaka watoto wangu na mimi.
“Lakini nimekuwa napambana na shida hizo huku nikimuomba Mungu, hauchihauchi unakucha,” alisema Irene huku akifuta machozi na kufafanua kuwa yeye ni mwenyeji wa Mbeya na kwamba wazazi wake ni wazee na hawawezi kumsaidia.
Aidha, aliongeza kuwa tangu ameondoka nyumbani kwa mumewe ndugu wa mume wakiwepo wakweze hawajahangaika kumtafuta, jambo ambalo linaashiria kuwa hatakiwi katika familia hiyo, lakini akadokeza kuwa ndugu zake wanaendelea kujichangisha ili waweze kumsaidia kwa chochote.
KWA NINI AKIMBIE NDOA?
Kwa mujibu wa Irene ni kwamba ndoa yake imekuwa na migogoro mingi huku akitaja mambo mengi zikiwemo imani za kishirikina.
Kutokana na kutopatikana kwa mume wa mwanamke huyo na kutopata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wakweze Irene, Risasi Jumamosi limezingatia weledi kwa kuhifadhi tuhuma hizo hadi pale watuhumiwa watakapopatikana na kupata maelezo yao pia.
MAMA MKWE AFUNGUKA
Baada ya jitihada nyingi kufanywa ili kujaribu kuweka sawa mizania ya habari hii, Risasi Jumamosi lilifanikiwa kumpata mama mkwe wa Irene ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake.
RISASI: Unamfahamu Irene? Lilikuwa swali lililofuata nyuma ya salamu, utambulisho na kufahamiana kidogo.
MKWE: Huyo simfahamu kabisa na sitaki kumfahamu, wa nini?
RISASI: Mbona anasema wewe ni mama mkwe wake?
MKWE: Ndiyo kajua leo, jana tu katoka hapa kunitukana na kuniita mimi mchawi leo hii anasema mimi mkwe wake!
RISASI: Kumbe Irene unamfahamu, sasa imekuwaje mwanao amfukuze mke wake na watoto na kuwaacha wanatangatanga mitaani?
MKWE: Muulize yeye au baba mkwe wake atakuwa anajua.
RISASI: Namba ya mumeo unaweza kunipatia ili nimuulize haya!
MKWE: Mwambie huyo aliyekupa hiyo habari akupe.
RISASI: Lakini mama hebu tuongee kiutu uzima, mkweo anaweza kuwa mbaya, lakini na hawa malaika mnaowatesa wamekosea nini? Kwa nini msikae nao mkawalea?
MKWE: Kwa aliyonifanyia huyo mama sitamsamehe kabisa na sitaki hata kuzungumza naye hadi nakufa.
RISASI: Nimekuuliza habari ya kuchukua watoto na kuishi nao unashwidwaje?
MKWE: Watoto hao sijaanza kuwalea leo, kuna kipindi waliokotwa Maili Moja (Kibaha- Pwani), nikaenda kuwachukua, sasa leo anaponiita mimi mchawi na kusema hawa watoto siyo wa mwanangu unataka mimi nifanye nini?
Hadi tunakwenda mtamboni mama huyo mwenye watoto wanne alikuwa akiendelea na maisha yake mitaani huku akilalamika kukosa chakula na nguo jambo ambalo linasikitisha.
Kwa mtu anayetaka kumsaidia Irene chochote anaweza kuwasiliana naye kwa namba 0658837801- Mhariri.
STORI: Shamuma Awadhi, Risasi Jumamosi