
MWIGIZAJI wa sinema za Kibongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’ ameona fursa ya kutangaza biashara ya filamu ni kubwa kwa sasa tofauti na kipindi cha nyuma, kwa kuwa utandawazi wa kujitangaza ni mkubwa. Akizungumza na Risasi Jumamosi, Dude alitiririka kuwa kwa sasa fursa ipo kutokana na vyombo vya habari kuwa vingi pamoja na mitandao ya kijamii kama Instagram, YouTube n.k.
“Zamani ilikuwa ni tofauti kabisa, kuna baadhi ya watu ndiyo walikuwa wananufaika kwa sababu kulikuwa na maharamia, unaweza kutoa kazi yako leo, lakini kesho na kesho kutwa unakuta kazi yako imesambaa Kigoma, Mwanza na mikoa mingine kabla wewe hujaitoa. “Lakini sasa ukiwa na kazi yako unaingiza kwenye chaneli yako ya YouTube inakuingizia kipato ndiyo maana hata wasanii wakubwa huwa wanafanya hivyo na hivi Serikali ipo na sisi kwa ajili ya kutushughulikia hati miliki huenda mambo yakawa poa zaidi,” alisema Dude