
MARA: BAADA ya kuwepo kwa visa na matukio mengi ya watu kujeruhiwa mkoani hapa, hivi karibuni tukio lingine baya limetokea na kutikisa wilayani hapa kwa watu watatu kujeruhiwa kwa vitu vyenye ncha kali na ‘ wasiojulikana; Uwazi lina mkasa mzima.
Chanzo cha habari kinasema mtu wa kwanza kuvamiwa na watu hao wabaya alikuwa ni Diwani wa Kata ya Kenyamanyori (CCM)] Halmashauri ya Mji wa Tarime, aliyejulikana kwa jina la Ganga Mgendi. Mgendi alishambuliwa na wasiojulikana saa 2 usiku wa Septemba 19, mwaka huu eneo la mgodi wa dhahabu wa Kibaga ambapo mbali na kujeruhiwa vibaya aliporwa vitu vyote zikiwemo fedha na simu.
ILIKUWAJE?
Inasemekana kiongozi huo wakati anarudi nyumbani kwake alipofika eneo la mgodi huo, ghafla kundi la watu lilimvamia na kuanza kumshambulia kwa kumkata mapanga sehemu mbambali za mwili. Wakati akiendelea kujihami kutoka mikononi mwa watu hao wasimuue; diwani huyo alikuwa pia akipiga yowe kuomba msaada wa majirani. Mungu alisaidia sauti yake ilisikiwa na mlinzi wa eneo hilo la madini aitwaye Monyeka Mwita ambaye aliacha lindo lake na kwenda kumsaidia Mgendi asiuawe.
Pamoja na kazi nzuri ya uokoaji aliyoifanya Mwita lakini naye alijikuta katika mtego wa wasiojulikana hao ambao walianza kumshambulia kwa silaha yakiwepo mapanga. Hali ya mapambano ilipozidi kuwa mbaya na eneo kutawaliwa na damu, Mwita akisaidia na diwani waliendelea kupiga yowe kuomba msaada zaidi ambapo alijitokeza kijana mwingine, Amosi Masunga kuja kuongeza nguvu.Hata hivyo, kundi hilo la wasiojulikana halikumuacha salama Amosi naye lilimshambulia kwa mapanga kisha watu hao kutokomea kusikojulikana na kuwaacha majeruhi wakiwa hoi.
WAPELEKWA HOSPITALI
Mara baada ya kundi hilo la wasiojulikana kutokomea, wasamaria wema wengine walijitokeza kuwachukua Mwita, Amosi na diwani na kuwapeleka Hospitali ya Tarime kwa ajili ya matibabu. Habari zinaeleza kwamba hali ya majeruhi hadi hivi sasa zinaendelea vizuri isipokuwa Diwani Mwita ambaye ametajwa kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, mkoani Mwanza kwa tiba zaidi.
UWAZI LAFIKA HOSPITALI
“Waliponipora wakaanza kunikatakata na mapanga kichwani na mgongoni, nikisikia wanasema kuwa tumetumwa kukuua.“Ninashukuru nilipopiga kelele wasamaria wema wakajitokeza kunisaidia, waliniacha na kukimbilia kusikojulikana” alisema Mgendi alipozungumza na Uwazi lililokwenda hospitali kumjulia hali.
Hata hivyo, diwani huyo alipoulizwa kuhusu kuwa na kisasi au uadui na watu, alikana na kuonesha kushangazwa na kushambuliwa kwake. Naye Mwita alipoulizwa hali ilivyokuwa siku ya tukio alisema: “Watu hao walikuwa zaidi ya wanne, mimi nilikuta wanamshambulia diwani nikawa namsaidia wasimuue, wakanigeukia na kuanza kunipiga kwa mapanga hadi nikaanguka chini, nikapipiga kelele, akaja Amos kutuokoa,” alisema Mwita.
Uwazi lilishuhudia pia idadi kubwa ya wananchi wa Kata ya Kenyamanyori ambao walifurika katika katika Hospitali ya Tarime kuwashuhudia majeruhi hao, huku wengi wao wakionesha kuchoshwa na matukio ya mara kwa mara ya watu kujeruhiwa. “Yaani sijui kuna nini? Unajua hali inatisha sana, matukio yamekuwa mengi sana, Tarime imekuwa ya kumwagana damu, nadhani tunatakiwa kubadilisha hii sura mbaya ya eneo letu.
“Watu wapewe elimu waambiwe zama za kale zimepita hizi ni zama mpya za kutumia akili zaidi ya nguvu za kukatana mapanga na sime,” alisema kijana mmoja liyejitaja kwa jina moja la Chacha. Uwazi lililotumia takriban saa mbili kuwepo hospitalini hapo na kufanya mazungumzo kadhaa na watu mbalimbali ambao wengine walionesha kuchoshwa na uwepo wa matukio ya watu kujeruhiana na kuuana au kutiana vilema vya maisha.
“Serikali iendelee kutafuta njia za kujenga jamii inayozunguka Mkoa wa Mara katika misingi ya kuheshimiana na kutojichukulia sheria mikononi, vinginevyo matukio ya namna hii yakiendelea itakuwa ndoto kuyakomesha,” alisema kijana mwingine ambaye hakutaka kuja jina lake. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime Rorya, SACP Henry Mwaibambe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba tayari watu kadhaa wamekamatwa kuhusiana na unyama huo.
STORI: IGENGA MTATIRO, UWAZI