
HALI ALIYONAYO mtoto Hamis Hashim, mkazi wa Yombo- Dovya jijini Dar bado ni mbaya ambapo hivi karibuni baada ya msanii wa filamu Bongo, Kajala Masanja kumtembelea, alijikuta akiangua kilio kutokana na uchungu aliopata. Habari ya Hamis iliandikwa na gazeti hili wiki iliyopita ikieleza kuwa, licha ya mwaka 2013 kupelekwa India kwa ajili ya matibabu, aliporejea hali iliendelea kuwa mbaya zaidi ya ilivyokuwa awali.
Katika habari hiyo, Hamis alieleza mazingira magumu anayoishi kutokana na tatizo alilonalo kwa miaka 10 sasa la kujaa miguu na akawaomba Watanzania wamsaidie kwa hali na mali.
Kufuatia kilio hicho cha Hamis, katikati ya wiki hii, Kajala alipiga simu kwenye chumba chetu cha habari na kueleza kuwa, ameguswa na tatizo alilonalo mtoto huyo na kwamba angependa kwenda kumtembelea.
RISASI, KAJALA KWA HAMIS
Kufuatia ombi la staa huyo, mwandishi wetu aliongozana naye hadi nyumbani kwa Hamis na kumkuta akiwa kwenye hali ya majonzi ambapo Kajala, baada ya kumuona, alianza kutokwa na machozi.
“Jamani jamanii….daaah! Eee Mungu msaidie mtoto huyu, kwa kweli inauma sana, lakini naamini kuna siku Mungu atatenda miujiza,” alisema Kajala aliyekuwa ameongozana na wafanyakazi wenzake wa Kampuni ya Kay Entertainment huku akitokwa machozi.
Kajala akasema ameguswa na tatizo la mtoto huyo, lakini anashindwa kujua aanzie wapi ili furaha irejee kwake. Hata hivyo, akasema, ameanza kumsaidia kwa kidogo alichokuwa amejaaliwa, lakini atahakikisha msaada atakaokuwa anahitaji, yeye kama Kajala atajitoa na kuhamasisha wengine wamsaidie.
“Nimewasiliana na madaktari wa Muhimbili ili kujua wapi tunatakiwa kuanza katika kumtibu, tayari wamenipangia siku ya kumpeleka ili tatizo lake lijulikane ni lipi hasa ili aweze kutibiwa na kama anatakiwa kwenda nje ya nchi tutajua pia,” alisema Kajala.
KUTOKA RISASI
Hamis kama picha zake zinavyomuonesha, anapita katika wakati mgumu mno. Anahitaji huruma yako wewe msomaji hivyo kama umeguswa na ungependa kumsaidia kwa namna yoyote, wasiliana nasi kwa namba 0719 489644, tutakufikisha kwake na utaona namna ya kumsaidia
STORI: Imelda Mtema, Risasi Jumamosi