×

Rais Autaka Umoja wa Mataifa Kutekeleza Maazimio Yake

GHANA imeutaka Umoja wa Mataifa kutekeleza maazimio ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ili kuufanya uendane na maslahi ya nchi zote husika.

 

Akizungumza kwenye mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Ghana, Nana Addo Dankwa Akufo-Addo amesema umoja huo unapaswa ama kuwa na ari ya kisiasa ya kutekeleza maazimio yake ya kuleta amani na usawa kwa nchi zote au ubakie kuwa kundi la nchi zenye kupitisha maazimio tu na halafu kupuuza utekelezaji wake.

 

Akisimulia kuanzishwa kwa umoja huo miaka 73 iliyopita (1945) huko San Francisco, Marekani, Addo alisema mazingira ya kuanzishwa kwake na yale yaliyopo sasa yana tofauti kubwa. Alisema hivi sasa kiuchumi dunia inatingishwa na nguvu za mataifa mawili makubwa duniani na hivyo kusababisha maslahi ya nchi ndogo duniani kama Ghana yasipewe kipaumbele.

 

Amesisitiza kuamini kwake kwamba dunia imejaa kila aina ya raslimali ambazo zingeweza kuleta maendeleo na ustawi kwa nchi zote duniani. “Hili linawezekana iwapo patakuwa na sheria na mazingira sawa ya kufanyia biashara na shughuli zote kwa nchi zote bila kupendelea nchi fulani,” alisema na kuongeza kwamba hilo linawezekana kwa kupitia Umoja wa Mataifa.

 

Akizungumzia moja kwa moja matatizo ya nchi changa, hususan za Afrika, alisema asilimia 55 ya kazi za Baraza la Usalama la umoja huo zinahusiana na Afrika katika kulinda amani na kukabiliana na umaskini.

 

“Hatutaki kuwa eneo lililojaa taasisi za kulinda amani na mashirika ya kupiga vita umaskini,” alisema na kuongeza kwamba jumuia za Afrika kama jumuia ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) na Umoja wa Afrika (AU) zinatosha na zitafanikiwa kudhibiti hali hiyo.

 

Kufanikiwa katika hilo, alisema, kinachotakiwa ni kuhakikisha Afrika inatoa kipaumbele cha kuwaelimisha na kuwapa mafunzo watu wake. Katika lengo hilo, alisema, nchi yake inashirikiana na mataifa mengine duniani, hususan China katika kujenga miundo mbinu ambayo itaifanya Ghana kuwa sehemu ya maendeleo na ustawi wa binadamu wote Afrika na duniani kote.

VIDEO: GARI, Pikipiki Vikitolewa Kwenye Maji Kuzama MV Nyerere