×

USAFIRI WA MAFIA NI HATARI MARA MBILI YA MV NYERERE  

MAZINGIRA ya usafirishaji abiria kupitia Bandari ya Nyamisati iliyopo Rufiji kwenda Mafia mkoani Pwani, ni hatari sana mara mbili ya kivuko kilichopinduka cha MV Nyerere huko Ukerewe, Mwanza.

Usafiri huo wa Mafia ukiende­lea hivyo unaweza kusababisha vifo vya watu wengi wenyeji wa kisiwa hicho.

Kisiwa cha Mafia kina historia ndefu na yenye kuvutia zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita inayoelezea mafungamano ya kibiashara kati ya kisiwa hiki na nchi ya Misri ya kale pamoja na miji mingine ya Mashariki ya Kati.

 

Pamoja na hayo, lakini kisiwa hiki wakazi wake wana hatari kubwa, hasa wale wanaolaz­imika kutoka nje ya kisiwa kwa sababu usafiri pekee rahisi ni wa kutumia vyombo vya usafiri vya baharini.

Wakizungumza na mwandishi wa makala haya baadhi ya wa­nanchi na watumiaji wa Bandari ya Nyamisati iliyopo Rufiji Mkoa wa Pwani, wanaeleza kwamba, hawapo salama kutokana na shaka tele inayotokana na mazingira mabovu ya bandari hiyo inayosafirisha watu na bidhaa mbalimbali kutoka bara kwenda Mafia.

 

Wananchi hao wanamwele­za mwandishi wa makala haya mengi walipozungumza kwa njia ya simu kwamba, maisha yao yamewekwa reheni na Serikali yao kutokana na kuto­jali usafiri ambao unatumiwa na wengi visiwani humo.

Mwakombo Issa, mmoja wa wasafiri hao aliyekuwa bandarini hapo anaeleza kuwa, amefika hapo mchana na kwamba, anasubiri usafiri wa boti iliyotarajiwa kuondoka saa tisa usiku, jambo am­balo linaonesha tatizo la safari kwenye kisiwa hiki.

 

Anasema kuwa, vyombo vinavyotumika kusafirishia abiria baharini ni duni na kwamba, boti hizo hazina usalama wa kutosha na zilivy­oundwa na pia hawana jaketi za uokoaji.

“Ufike muda wowote, lakini kuondoka ni usiku, tena usiku wa manane, likiwafika jambo mkiwa baharini, ni vigumu kupata msaada kwa kuwa, muda huo wahusika wana­kuwa wamelala,” anasema.

Saidi Maboko naye anasema kuwa, mtu akisafiri kwenda Mafia kupitia bandari hiyo ya Nyamisati, hulazimika kuweka kambi bandarini hapo.

 

Na kwamba, eneo hilo si rafiki kwa usalama na afya za wasafiri kutokana na mbu kuwa wengi, baridi nayo ni kali, lakini pia hatari ya kush­ambuliwa na wanyama wakali.

“Kwa kweli watu wa Mafia tunateseka katika usafiri kwa muda mrefu, kila siku tunasikia viongozi wa kisiasa wakileta porojo kwamba watamaliza tatizo hili.

“Hapa watoto wengi wa­nateseka na wanapata malaria hapahapa. Kwa kweli hii ni aibu, tangu tupate uhuru hatuja­wahi kusafiri kwa raha sisi watu wa Mafia,” anasema Maboko.

 

Mwananchi mwingine, Khadija Mohammedi Hus­sein anasema watu wa Mafia wamechoshwa na majivuno ya wanasiasa majukwaani na kutofanya mambo kwa vitendo kwani jamii inateseka kwa muda mrefu katika usafari.

Lakini Diwani wa Kata ya Kilin­doni, Mafia Ahamadi Mbonde, alipohojiwa anasema kuwa, ingawa yeye ni miongoni mwa watumiaji usafiri huo, lakini hali si salama.

“Kwanza boti zinaondoka katika wakati mbaya yaani nyakati za usiku, mathalan kumetokea ajali wakati huo ni ngumu kupata msaada,” anasema Diwani Mbonde.

 

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Shaibu Mnunduma akizun­gumza na mwandishi wetu anasema eneo la Bandari ya Nyamisati linahusiana na Wilaya ya Rufiji na kwamba, kutokana na watu wanaotumia bandari hiyo kuwa ni watu wa wilaya yake, alizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Rufiji ili kushughulikia matatizo hayo.

Baadhi ya wananchi wanahoji, Kisiwa cha Mafia kimelaaniwa na nani? Mbona kila kiongozi anayekuja anawadanganya?

 

Mwaka 2015 ulikuwa ni wa uchaguzi mkuu wakamchagua Mbunge wa Mafia, Mbaraka Kit­wana Dau, miongoni mwa ahadi zake na utekelezaji wake ni kuleta kivuko, meli au boti ya kisasa kutoka Nyamisati, Rufiji hadi Ma­fia, Kilindoni, lakini wanadai kuwa mpaka leo hakuna boti wala meli mpya.

Badala yake wananchi wanaendelea kusafiri na usafiri uleule wa zamani wa MV Mafia Line, Mafia Raha, Julie na Shell. Hakuna ubishi kwamba boti hizo ni za kale na hazikidhi kwa kusafirisha wananchi wa visiwa hivyo.

 

Ipo wapi boti ya kisasa? Ipo wapi meli ya kisasa? Ni maswali ya wananchi wa Mafia.

Hata hivyo baadhi ya wananchi walioongea na Uwazi juzi walim­womba Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Mhandisi Isack Kamwelwe kuwapelekea boti ya kisasa ili kuwaondoshea hatari inayowanyemelea.

MAKALA: ELVAN STAMBULI

BREAKING: MHANDISI WA MV NYERERE AOKOLEWA AKIWA HAI – VIDEO