MWIMBAJI wa nyimbo za Injili Bongo, Irene Mwamfupe amesema anatarajia kufanya uzinduzi mkubwa wa albam yake inayokwenda kwa jina la Hodari.
Uzinduzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 25, mwaka huu, utapambwa na waimbaji wakubwa wa muziki wa Injili akiwemo Bahati Bukuku, Happy Milinga, Mariam Kilyenyi, Martha Mwaipaja, Mchungaji Bony Mwaitege na Edda Mwampanga.
Akiuzungumzia uzinduzi huo utakaofanyika ndani ya Kanisa la Mito ya Baraka, Kariakoo jiini Dar, Irene alisema siku hiyo ambayo itakuwa ni Jumapili, itakuwa ni siku njema ya kumsifu Mungu na itakuwa ni siku ya kupokea miujiza kupitia sifa.
“Mungu wetu hukaa katikati ya sifa kwa hiyo Jumapili hiyo atakaa katikati yetu na tutapokea mahitaji yetu kwa sababu tumeacha vyote na kujumuika pamoja kumsifu Yeye Bwana.
“Niwakaribishe watu wote, hakutakuwa na kiingilio, waje washuhudie uzinduzi wa albam yangu ya Hodari na pia wataweza kuwasikia na kuwaona wanamuziki wenzangu wa muziki wa Injili,” alisema Irene.
Irene alisema mbali na waimbaji hao, waimbaji wengine watakaoupamba uzinduzi wake ni pamoja na Emmanuel Mgaya ‘Masanja’, Emmanuel Mbasha, Madam Ruth, Miriam Mauki, Joyce Ombeni, Tumaini Mbembela na Tumaini Msowoyo.
Orodha haijaishia hapo, atakuwepo pia Chris Mwahangila, Martha Baraka, Isingo Mwaisingo, Ritha Komba, Sarah Mvungi, Upendo Kihayile, Heri Mboya, Daina Sakatebela, Loyce Nducha na Elizabeth Eliah.
Pia zitakuwepo kwaya zote za Mito ya Baraka ambazo ni Jerusalem Choir, Rhema Kwaya, Ebenezer Kwaya, WWI Kwaya na The Joshua Generation.
STORI: OVER ZE WEEKEND, DAR