×

YUPO WAPI BADI BAKULE? MSIKIE AKIFUNGUKA AKLIVYOPOTEA

KAMA kawaida ya safu kila wiki inakuletea wasanii mbalimbali ambao walitamba kwa kipindi fulani na kuwa gumzo kila kona lakini kwa sasa wamepotea.

Kama wasomaji na mashabiki wengi walivyotaka kujua, leo tunakuletea mwanamuziki, Badi Bakule aliyewahi kutamba na bendi mbalimbali ikiwemo African Revolution ‘Wana Tamtam’, ToT, African Stars ‘Twanga Pepeta’ na nyingine nyingi.

 

Badi Bakule ameeleza mengi kuhusiana na kupotea kwake, ungana naye hapa chini;

Risasi: Mashabiki wako wangependa kujua safari yako ya muziki ilianza vipi?

Bakule: Nilianza kupenda kazi ya muziki tangu nikiwa mdogo lakini niliingia rasmi kwenye fani hii mwanzoni mwa miaka ya tisini kupitia Bendi ya Rola Africa ambayo ilikuwa Manzese Midizini, Dar.

Risasi: Ulikaa kwa muda gani kwenye Bendi ya Rola?

 

Bakule: Nilikaa kwenye bendi hiyo kwa muda mfupi kwa kuwa nilikuwa katika safari ya kusaka mafanikio nilihamia kwenye bendi za ADR Stars ya Manzese na kuanzia hapo ndiyo nikaanza dili nyingi za mbali.

Risasi: Ulipata dili za mbali kama zipi?

 

Bakule: Nilifa-nikiwa kujiunga na Bendi ya Jailani ya Moshi mkoani Kilimanjaro kisha kupata dili lingine mkoani Arusha katika Bendi ya Sayari. Sikuishia dili za hapa Bongo nilipata kazi nchini Kenya ambapo nilifanya kazi na bendi tofauti hali ilinifanya hata niliporudi hapa nchini nifikie kwenye bendi ya kueleweka.

 

Risasi: Baada ya kurudi nchini ulijiunga na bendi gani ya kueleweka?

Bakule: Nikiwa Kenya nilianza kusikia muziki wa dansi Bongo ukiwa juu hivyo niliporudi nilifikia kwenye Bendi ya African Revolution ‘Wana Tamtam’ iliyokuwa ikimilikiwa na African Stars Entertainment (ASET) ambapo nilitunga nyimbo kadhaa zilizonipatia umaarufu kama vile, Kijino Pembe, Chande, Maya, Usia wa Baba na nyingine nyingi.

 

Risasi: Uko kimya sana, tatizo ni nini?

Bakule: Baada ya kuona muziki wa dansi unasuasua niliamua kupumzika na kurudi kwetu Ruvu kuangalia kazi nyingine.

Risasi: Je, huko kwenu sasa unafanya kazi gani kuendeleza maisha?

Bakule: Ninafanya biashara zangu na ninaona maisha yanazidi kunoga kila kukicha.

Risasi: Una mpango wa kuwika tena kimuziki?

 

Bakule: Licha ya kwamba nimepotea kwa miaka mingi huku nikiendelea na biashara, nimeanzisha bendi yangu inayoitwa Sayari na tayari ina nyimbo mbili tutaanza kurekodi hivi karibuni zinazoitwa Pete ya Ndoa na Kiuno Feni.

Risasi: Hiyo bendi yako ipo kwenu Ruvu au wapi?

 

Bakule: Bendi yangu makao yake yapo Manzese, Dar na nimewachukua wakongwe wenzangu kama Rogat Hegga ‘Katapila’ na Hadija Mnoga ‘Kimobitel’.

Risasi: Ni mafanikio gani umeyapata kwenye muziki?

Bakule: Muziki umeniwezesha kujenga nyumba maeneo ya Mbezi Kwa Msuguri. Faida nyingine kubwa ameweza kwa na familia yenye watoto watatu.