DAR ES SALAAM: Raia wa kigeni (Mzungu) amenaswa laivu akionesha mahaba ya aina yake kwa dada yetu wa Kibongo aliyefamika kwa jina moja la Semeni, mkazi wa Mwananyamala jijini Dar.
Tukio hilo la amshaamsha lilijiri mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Klabu ya Masai iliyopo ndani ya Hoteli ya Meriadian, Mwananyamala jijini Dar ambapo Bendi ya Bogoss Musica ilikuwa ikifanya makamuzi chini ya prezidaa wake, Nyoshi El Saadat.
Katika tukio hilo lililoshuhudiwa kwa macho makavu na Ijumaa, burudani ikiwa imenoga, Semeni ndiye aliyeanza kuingia sehemu ya kuchezea (dance floor) ndipo mtasha huyo baada ya kuvutiwa na mikogo yake alimfuata na kuanza ‘kukonki konki’ (kuserebuka) naye kimahaba.
Staili waliyokuwa wakitumia wawili hao ilionesha dhahiri shairi kuwa mtasha huyo alikuwa amekolea kimahaba kwa mdada huyo wa Kibongo ambaye wenzake walikuwa wakimpongeza kwa ‘kuokota dodo chini ya mti wa muarobaini’.
Mashabiki wengine walikuwa wakicheza kwa kuachiana nafasi, lakini wawili hao walionekana kugandana kimahaba huku mtasha mwingine aliyekuwa pembeni yao akionekana kuwapa sapoti kwa kucheza pembeni yao kama anawalinda.
Mdada huyo ambaye alionekana kutomlazia damu mtasha huyo naye alionekana kuzidi ‘kumroga’ jamaa huyo kwa kumkatia viuno vya Kibongo ambavyo vilionekana kuzidi kumchanganya akili shemeji yetu huyo kutoka ughaibuni.
Mwanahabari wetu alitaka kuzungumza na wawili hao, lakini kutokana na kuzidiwa na uhondo wa burudani walimuonesha ishara ya kutaka waachwe waendelee kustarehe na hatimaye walitoweka ukumbini hapo.
Shuhuda mmoja aliyekuwa ukumbini hapo alisikika akimsifia mrembo huyo na kusema akiendelea kumkoleza kwa staili hiyo, mtasha huyo hawezi kupindua ni lazima atangaze ndoa.
“Yaani kwa mikato hii ya Kibongo dada yetu anayompa huyu mtasha hawezi kupindua kabisa, kama hana ndoa ni lazima atatangaza ndoa hapahapa Bongo,” alimalizia shabiki huyo kabla ya burudani kufikia tamati na kila mtu kurejea kwake.
Stori: Richard Bukos, Ijumaa.