The House of Favourite Newspapers

RAIS MAGUFULI AZINDUA MRADI WA MAJI JIJI LA ARUSHA (Picha +Video)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akivuta utepe pamoja na Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa Maji safi na usafi wa Mazingira katika jiji la Arusha. Wengine katika picha ni Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Isaack Kamwelwe pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB Alex Mubiru.

 

Rais John Magufuli leo Desemba 2, 2018 amezindua na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa visima vikubwa vya maji zaidi ya 20 jijini Arusha.

Rais amesema kuwa mradi huo utakaogharimu shilingi bilioni 520, unahusisha visima vya kuchimbwa na kumaliza tatizo la maji katika Jiji hilo, na zimekopwa katika Benki ya Maendeleo ya Afrika, hivyo zitalipwa na Watanzania wote kupitia kodi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia maji yanayotoka katika moja ya visima virefu vilivyopo katika mradi huo mkubwa wa maji safi na usafi wa mazingira katika jiji la Arusha. Mradi huo utakapokamilika utaweza kuzalisha lita za ujazo milioni 200 kwa siku tofauti na sasa ambapo lita za ujazo ni 45 milioni wakati mahitaji ya jiji la Arusha ni lita za ujazo milioni 90.

 

“Serikali imekopa bilioni 520 kutoka Benki ya maendeleo ya Afrika, kwa ajili ya Arusha ili kutekeleza mradi wa maji, hizi hela zitalipwa na Watanzania wote, na tumezileta kwa wale wale wanaoitukana serikali, na yote ni kwasababu maendeleo hayana chama”, amesema Rais Magufuli.

 

Rais Magufuli  akiendelea kuangalia maji  katika moja ya visima virefu vilivyopo katika mradi huo.

 

Aidha Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Isack Kamwele kutosita kuwafukuza wakandarasi wakishindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati, “Waziri usiogope kufukuza wakandarasi, kumbuka hata mimi nimewahi kuwa Waziri wa Ujenzi na sikusita kutimua wakandarasi wasiotekeleza miradi, wakaanza kuniombea laana, na hazikunipata kwakuwa Mungu anapenda maendeleo ya haki, wewe fukuza tu”.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema mradi huo ukikamilika uhaba wa maji Jiji la Arusha utapungua kwa kiasi kikubwa.

Rais Magufuli akizungumza jambo na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB Alex Mubiru wakati wa mkutano na wananchi wa Arumeru jijini Arusha mara baada ya kuzindua mradi huo wa maji
Rais Magufuli akizungumza na wananchi wa Arumeru mara baada ya kuweka jiwe la msingi mradi wa Maji safi na usafi wa Mazingira katika jiji la Arusha
Wananchi wa Arumeru wakishangilia wakati wa hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika kijiji cha Kimnyaki Arumeru.
Rais  Magufuli akisalimiana na Meya wa jiji la Arusha Calist Lazaro mara baada ya kuwahutubia wananchi wa Arumeru.

PICHA NA IKULU

 

Comments are closed.