Wagombea Uchaguzi Yanga Wahofia Kufanya Kampeni
KAMPENI za wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika Klabu ya Yanga zilizopangwa kuanza jana Alhamisi, zimeahirishwa baada ya wagombea kuhofia usalama wao.
Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imalize kuwafanyia usaili katika kuelekea uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Januari 13, mwaka huu.
Wagombea hao waliopitishwa na TFF wamekumbana na ugumu kutoka kwa wanachama wa Klabu ya Yanga ambao wanawatuhumu kuwa ni wasaliti baada ya kukubali uchaguzi wao usimamiwe na shirikisho hilo.
Juzi Jumatatu katika kikao cha viongozi wa Kata Tano za Matawi ya Yanga ya jijini Dar es Salaam kilichofanyika kwenye makao makuu ya klabu hiyo Jangwani, Dar yalitolewa mapendekezo kwa wagombea hao wote kufutwa uanachama baada ya kukiuka katiba ya Klabu ya Yanga.
Kikao kiliongozwa na mwenyekiti wa Kanda ya Dar, Shabani Uda ambaye pia ni Katibu wa Tawi la Manzese ambaye alisikika akisema: “Hatutakwenda kupiga kura siku ya uchaguzi kama TFF waking’ang’ani kuendelea kutusimamia uchaguzi wetu.”
“Ikumbukwe kuwa tangu TFF ilipotangaza kuendelea na mchakato wa uchaguzi wa Yanga bila kuwahusishwa viongozi wa timu hiyo, tahadhari ilitolewa juu ya uwezekano wa mchakato huo kukamilika kwani wenye uamuzi wa mwisho ni wanachama wa klabu kupitia katiba yao.
Comments are closed.