
SIMBA usiku wa kuamkia leo, imepoteza mchezo wa pili ugenini nchini Misri, kwenye hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba ilikumbana na kipigo cha mabao 5-0 kipindi cha kwanza dhidi ya Ahly kwenye mjini Alexandria mbele ya mashabiki 10,000 waliokuwa wakishangilia kwa kelele za hali ya juu mwanzo mwisho.
Ahly katika mchezo wa jana magoli yao karibu yote yalikuwa ya kideoni huku wakipiga pasi mpaka 15 mara kadhaa kabla ya Simba kuunasa mpira.

Katika mchezo wa jana, Simba ilianzisha mastaa wake karibu wote golini akisimama Aishi Manula,ukuta ulikuwa na Nicholas Gyan, Asante Kwasi,Paschal Wawa na Juuko Murshid. Wengine walioanza jana ni James Kotei, Rashid Juma, Jonas Mkude, Kagere, Okwi na Chama.
Kipindi cha pili angalau hawakuruhusu bao huku mastraika wa Simba Meddie Kagere na Emmanuel Okwi maji yakizidi unga.
Katika mchezo huo, Simba ilionekana kuzidiwa idara zote hususani kwenye safu ya ulinzi, hali ya hewa ya baridi nayo ikichangia kwani baadhi ya wachezaji walikuwa wamevaa jezi za mikono mirefu na glovu mikononi.
Matokeo hayo yanamaanisha kwamba Simba itakuwa imesaliwa na mchezo mmoja wa ugenini dhidi ya JS
Saoura kwani tayari ilishacheza na AS Vita na kufungwa mabao 5-0. Kwa mujibu wa kundi lilivyo, bado Ahly wataendelea kuwa vinara lakini salama pekee ya Simba kufuzu robofainali ni kushinda mechi zake mbili za nyumbani dhidi ya Ahly na Vita.
JS SAOURA YAAMBULIA SARE
JS Saoura jana iliwabana vilivyo AS Vita jijini Kinshasa na kutoka nao sare ya mabao 2-2 jambo ambalo limefufua matumaini yao kwenye msimamo wa kundi hilo. Saoura walitoka nyuma na kusawazisha mabao hayo na kufi kisha pointi mbili.