
UNAWEZA kusema wenye ligi yao wamerudi kutokana na kwamba jana Alhamisi, Simba ilicheza kwa mara ya kwanza mechi ya Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kupita takribani siku 40 na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo wa jana ambao kwa Simba ni wa 15 msimu huu kwenye ligi hiyo, mabao yao yalifungwa na Meddie Kagere dakika ya 20, Mzamiru Yassin (dk 25) na John Bocco (dk 29).

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alionekana kuingia na mfumo tofauti kidogo ili kuwachanganya wapinzani wake kutokana na kumuanzisha benchi mshambuliaji wake tegemeo, Emmanuel Okwi, kiungo Jonas Mkude na beki, Juuko Murshid. Wachezaji hao wamekuwa wakianza kikosi cha kwanza mara kwa mara.
Ushindi huo wa Simba umeifanya kufikisha pointi 36 na kushika nafasi ya tatu katika msimamo ikiwa imezidiwa pointi 19 na vinara ambao ni watani zao wa jadi, Yanga wenye pointi 55.

Yanga mbali na kuwapiku Simba pointi hizo, pia wamewazidi michezo ambapo vinara hao wamecheza mechi 22, wakati Simba wamecheza 15.
Endapo Simba ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo wataendeleza mwendo wake wa ushindi hadi kwenye mechi zake za viporo, basi wanaweza kukaa juu ya Yanga kwa tofauti ya pointi mbili.

Ikumbukwe kuwa, kwa muda mrefu Simba ilikuwa haijacheza mechi zake za ligi kuu kutokana na kuwa na mechi mfuatano za mashindano mbalimbali ikiwemo Kombe la Mapinduzi, SportPesa Cup na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mara ya mwisho kwa Simba kucheza mechi yake ya ligi msimu huu ilikuwa Desemba 29, mwaka jana ambapo ni dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Taifa na Simba ikaibuka na ushindi wa mabao 3-0. Bocco alifunga moja na Shiza Kichuya ambaye kwa sasa ametimkia kucheza soka nchini Misri, alifunga mawili.
Stori na Said Ally, Dar es Salaam | Picha na Musa Mateja
