×

Zahera Aichangia Yanga Mamilioni

Kocha mkuu wa timu hiyo Mkongomani, Mwinyi Zahera.

KLABU ya Yanga tayari imefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh milioni 21.3 kupitia kampeni yao ya kuichangia timu hiyo iliyoanzishwa mwezi huu. Kampeni hiyo ilianzishwa na kocha mkuu wa timu hiyo Mkongomani, Mwinyi Zahera aliyoianzisha kutokana na mtaji mkubwa wa wanachama waliopo Yanga.

 

Zahera alianzisha kampeni hiyo baada ya timu hiyo kuyumba kiuchumi tangu aliyekuwa mwenyekiti wao, Yusuf Manji kutangaza kujiuzulu.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa fedha hizo wamezipata kupitia michango wanayoichangia kupitia njia tatu za makampuni ya simu pamoja na benki. Saleh alisema, kwa kupitia Tigo Pesa wanachama wamechangia Sh milioni 5.9, M-Pesa milioni 6.3 na Benki ya CRDB Sh milioni 9.1.

 

Aliongeza kuwa, licha ya wanachama hao kuchangia, lakini bado hawajafikia malengo yao wanayoyahitaji, hivyo wamewaomba wanachama kuendelea kuichangia timu hiyo ili kufanikisha baadhi ya mahitaji yao.

 

“Tuanze kwa kuwashukuru wanachama wa Yanga kwa juhudi zao wanazozifanya katika kufanikisha malengo ya timu yao kwa kuichangia. “Licha ya michango hiyo kuipata kwa mwezi huu, lakini bado malengo hatujayafikia na badala yake wasi choke waendelee kuichangia timu katika kuiunga kampeni ya kocha wetu Zahera.

 

“Yanga ni klabu kubwa yenye mtaji mkubwa wa mashabiki kwa kupitia idadi hiyo kubwa ya mashabiki, Yanga inaweza kujiongoza yenyewe kwa kufanikisha baadhi ya mahitaji yao katika kipindi hiki kigumu ambacho inacho Yanga,” alisema Saleh.

Stori: Wilbert Molandi na Marco Mzumbe