×

Serengeti Boys Itumie Vizuri Safari ya Uturuki

KIKOSI cha timu ya vijana cha Tanzania, Serengeti Boys kwa sasa kipo nchini Uturuki kwa ajili ya michuano maalum ya UEFA Assist ambayo ilianza jana Jumamosi nchini humo. Serengeti Boys ambao wameonekana kuwa na morali ya hali ya juu katika miezi ya hivikaribuni wamealikwa katika michuano hiyo na kupangwa kundi moja na wenyeji Uturuki ambao ni miongoni mwa timu ngumu.

 

Timu nyingine za Afrika zilizoalikwa katika michuano hiyo ni Angola, Morocco, Uganda, Nigeria, Senegal na Guinea ambazo pia zitashiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana (Afcon) zitakazofanyika hapa nchini baadaye mwaka
huu huku matumaini ya kila Mtanzania yakiwa kwa Serengeti ambao wameonyesha kila dalili kwamba wanajua nini kinatarajiwa. Katika michuano hiyo ya Afcon, Serengeti Boys pia itashiriki na ndiyo itakuwa timu mwenyeji.

Hata hivyo, timu hiyo imekuwa ikifanya vyema katika michuano ya tofauti ambayo imekuwa ikishiriki hivi karibuni hali ambayo imesababisha Watanzania wengi kuwa na imani nayo. Imekuwa kwenye maandalizi kwa muda na iliweka kambi yake jijini Dar kisha Arusha kwa kufuata hali ya hewa ambayo kidogo inaendana na ile ya Uturuki.

 

Maandalizi ambayo wamefanya kule Arusha tunaamini yatakuwa msaada kwa timu hiyo katika michuano hiyo ambayo kwao itakuwa ni kipimo tosha kuelekea kwenye Afcon kwavile ina wababe karibu wote wa Afrika. Katika michuano hiyo ya UEFA, Serengeti itakutana na timu za kutoka Ulaya na Afrika ambazo zitakuwa ni kipimo tosha cha nini Watanzania watarajie kwenye michuano ijayo.

Ni matumaini yetu kwamba vijana hao watapambana kwa nguvu zao zote kwa kuona kuwa timu hiyo inaibuka kidedea kwenye michuano hiyo kama ambavyo ilifanya vizuri katika michuano Cecafa na Cosafa ambayo pia ilikuwa na ugumu wa aina yake kutokana na ugumu wa timu shiriki na maandalizi yao.

 

Haikuwa kazi rahisi na ndio maana hata waandaaji walikiri kwamba kweli Tanzania inaelekea pazuri kwenye soka la vijana. Wachezaji 20 ambao wamekwenda kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano hiyo ya Uturuki tuna hakika hawataiangusha nchi yetu kwani tayari viongozi wao na wadau wameshawaeleza mtihani mkubwa ulio mbele yetu Kitaifa.

 

Kila kheri Serengeti Boys kwenye michuano hiyo ya UEFA, mkapambane Watanzania tupo nyuma yenu kwa kila namna. Tunaamini kwa ufanisi wa Serengeti kwenye michuano hiyo utasaidia pia kuwatangazia nyota hao kimataifa na kufungua soko lao mapema kwani mawakala wengi watakuwepo kuangalia vipaji.

 

Ndio njia nzuri ya wachezaji wetu kujinadi kimataifa na kutafuta soko mbadala kuelekea walipo kina Mbwana Samatta na wengineo kwenye soka la kulipwa. Wana kila sababu ya kutumia vizuri nafasi hiyo kwavile umri unaruhusu na kiwango nacho kinaruhusu kufanya mambo makubwa. Hizo ndiyo nafasi adimu ambazo hutumiwa na wachezaji wa Ulaya walioko kwenye madaraja ya chini kujiuza machoni mwa klabu kubwa.