×

GEITA: MAPACHA WALIOZALIWA WAMEUNGANA WAFARIKI

Watoto mapacha waliozaliwa wakiwa wameungana katika Hospitali ya Rufaa Geita, wamefariki dunia wakiwa njiani wakipelekwa Hospitali ya Rufaa Bugando. Watoto hao walizaliwa na Theodora Wilson ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Kasuguya, wilayani Nyang’wale mkoani Geita, Machi 17 mwaka huu.

 

Mama huyo ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Kasuguye Kata ya Bukwimba Halmashauri ya Msalala, alijifungua watoto watatu wa kike kwa mpigo huku wawili hao wakiwa wameungana. Muuguzi mfawidhi wa Hospitali hiyo, Charugamba Jackson athibitisha kutokea kwa msiba huo.

 

Siku baada ya kujifungua, Theodora alisema kuwa, mtoto wa kwanza alijifungua kawaida ila baada ya hapo alisikia maumivu makali mno tumboni ndipo akaomba kupimwa na kukuta kuna watoto wengine ambao ililazimika afanyiwe upasuaji ili watolewe.

 

Alisema madaktari walimwambia watoto hao wanaweza kutenganishwa kwa sababu kila mtoto ana viungo vyake hivyo haoni kama hilo ni tatizo la kumfanya ashindwe kuwalea watoto hao kama anavyowalea watoto wengine, lakini leo Mwenyezi Mungu amewachukua.