
MKURUGENZI wa Mipango wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthum Mansoor, aliyetajwa jana, Machi 28, 2019 na Rais Dkt. John Magufuli kuwa anatuhumiwa kuwadhulumu fedha wafanyakazi wa taasisi hiyo kwa kuwaahidi kuwapatia viwanja na asifanye hivyo, amekamatwa na polisi.
Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, Kulthum alikamatwa jana Alhamisi Machi 28, 2019 na kupelekwa kituo cha polisi cha Oyster Bay, jijini Dar es Salaam ambapo leo Ijumaa Machi 29 atafikishwa mahakamani.
Akizungumza jana Ikulu baada ya kumuapisha Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Valentino Mlowola, rais alisema kuna mkurugenzi mmoja wa makao makuu Takukuru aliyewauzia viwanja hewa wafanyakazi wenzake, lakini alishangaa mtu huyo kutopelewa mahakamani.
“Wala sijapata taarifa kwamba hizo fedha amezirudisha kwa wafanyakazi aliowadhulumu. Wafanyakazi wanaumia, wanalalamika pembeni. Amewadanganya kwamba ana viwanja Bagamoyo, lakini mpaka leo hawajapewa,” alisema Magufuli.
Aliongeza kwamba kashfa hiyo iliibuliwa tangu Balozi Mlowola alipokuwa mkurugenzi wa taasisi hiyo, lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.
“Suala hili lilianza tangu wakati wa Balozi Valentino, nikamuuliza huyu mbona harudishi fedha au hapelekwi mahakamani, akawa na kigugumizi, sasa na wewe usiwe na kigugumizi kwa sababu nafasi za ubalozi zimeisha. Ndiyo maana huwa najiuliza hawa Takukuru huwa ni kwa ajili ya watu wengine, wao ‘hawaji-takukuru’ humohumo ndani?” alihoji.