INAHUZUNISHA! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mama mzazi wa aliyekuwa staa mkubwa wa filamu za Kibongo, Steven Charles Kanumba ‘The Great’, Flora Mtegoa kuzimia kwenye kaburi la mwanaye huyo alipokwenda kwenye misa ya kumbukumbu ya miaka saba tangu ampoteze mwanaye huyo.
Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012 baada ya kuanguka akiwa nyumbani kwake Sinza-Vatican jijini Dar.
Akizungumza na Risasi Jumamosi, mama huyo ambaye alifanya kumbukumbu ya Kanumba ambaye ametimiza miaka saba tangu afariki dunia, alisema kuwa mwaka huu alipokwenda kaburini kwa mwanaye huyo alijikuta akilia hadi anazimia ambapo aliongozana na wasanii wachanga, tofauti na miaka ya nyuma walipokuwa wakihudhuria mastaa wakubwa.
“Niliongozana na wasanii wachanga tu kutoka Tabata ambao miaka ya hivi karibuni ndiyo nimekuwa nikishirikiana nao, lakini hakuna staa yeyote aliyekuja kuungana nami na mimi namshukuru Mungu kwa kunipa umri mrefu kwani napata nafasi ya kumuombea mwanangu aendelee kupumzika kwa amani,” alisema Mama Kanumba.
Akieleza sababu ya kuzimia kwake, mama huyo alidai kuwa alijikuta akipata uchungu na kulia mno baada ya msanii mmoja chipukizi kuimba wimbo wa marehemu Kanumba ambapo aliimba huku akipiga gitaa, kitendo kilichowaliza wengi.
“Niliwahi kusema sitalia tena, lakini kwa huyo kijana alivyoimba nilishindwa kujizuia kabisa, nikalia sana mpaka nikazimia,” alisema mama huyo.
Kanumba alizikwa kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar ambapo umati mkubwa ulihudhuria tofauti na watu wote waliowahi kutangulia mbele ya haki kwani kifo chake kilishtua wengi.
Mungu ailaze roho ya Kanumba mahali pema, peponi, Amen.-Mhariri.
Stori: Imelda Mtema, RISASI MCHANGANYIKO