UNAMKUMBUKA Dkt. Louis Shika? Yule wa ‘Milioni 900 Itapendeza?’ Unakumbuka gumzo lake? Basi yeye ni cha mtoto, yupo mtu aliyevunja rekodi ya Dk Shika ambaye anatikisa kwenye mitandao ya kijamii, Peter Gumbo ‘Pierre Konki Liquid’.
Dk Shika aliibuka baada ya kutangaza dau la shilingi milioni 900 katika mnada wa nyumba za mfanyabiashara Said Lugumi zilizokuwa zikipigwa mnada na Kampuni ya Udalali ya Yono chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zilizokuwa Mbweni, Wilaya ya Kinondoni na Upanga Wilaya ya Ilala, Dar.
Hata hivyo, baadaye iligundulika kuwa Dk Shika ambaye mbali na nyumba hiyo ya shilingi milioni 900, pia alitangaza dau la shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kununua nyumba nyingine iliyokuwa Mbweni kisha baadaye kutaka kununua nyumba nyingine iliyokuwa Upanga kwa shilingi bilioni 1.2, hakuwa na fedha, kwani alipotakiwa kulipa asilimia 25 ya fedha hizo kama utaratibu ulivyoelekezwa awali, alishindwa kufanya hivyo.
Jina lake lilipaa na kumfanya ajulikane kiasi cha kufanya matangazo kadhaa ya biashara na baadaye kuonekana akishiriki kwenye video ya wimbo wa Kundi la Rostam, linalowaweka pamoja wasanii Roma na Stamina.
REKODI YA PIERRE
Tofauti na Dk Shika, moto wa Pierre umeonekana kuwa mkali zaidi, hasa baada ya jina lake kupaa kwa kasi ya moto wa petroli kiasi cha kupata mialiko katika vyombo mbalimbali vya habari, nje ya mitandao ya kijamii. Tayari ameshafanya ziara nchini Kenya ambapo kabla ya kwenda kwenye shoo, alihojiwa na redio mbalimbali za nchini humo.
NJE YA AFRIKA MASHARIKI
Katika kuonesha kuwa Pierre ameivunja rekodi ya Dk Shika ambaye enzi za umaarufu wake, alipanda ndege hadi mjini Shinyanga alipoalikwa kama mgeni rasmi kwenye mahafali ya wanafunzi wa Chuo cha Afya Kahama (Kahama College of Health Science), Novemba 23, 2017, Pierre yeye ameshatembelea nchi za Afrika Mashariki na sasa anajiandaa kwenda Marekani.

Lucas Kinyenda, mkazi wa Sinza jijini Dar, alipozungumza na Risasi Mchanganyiko, alisema kuna tofauti kubwa kati ya Dk Shika na Pierre. “Pierre yeye amekuja kwa staili ya peke yake. Ingawa ametambulishwa na vituko vyake vya ulevini, lakini utaona kama anavutia watu na anaonekana anaweza kuwa msanii mzuri wa komedi.
“Kwa upande wa Dk Shika, watu walikuwa wakivutiwa na namna yake ya kujiaminisha kutaka kununua nyumba, wakati uwezo huo hakuwa nao. Kwa tukio hilo isingewezekana kudumu kwa muda mrefu.
“Watu walimfuatilia muda mrefu wakiamini labda huenda hizo fedha zake alizokuwa akitamba zingeingia nchini muda wowote, labda kweli zingeingia, lakini walipoona mwelekeo hakuna, wakampotezea. Ni tofauti kabisa na Pierre ambaye anaonekana kumpoteza jumla,” alisema Kinyenda.
Safari ya Pierre kwenda Marekani iliyopo mbele yake, ni mwaliko wa sherehe za Tanzania Day ambayo imeandaliwa na Watanzania waishio nchini humo. Mbali na Marekani, pia atakaporejea anatarajia kwenda jijini London, Uingereza ambapo amealikwa na mchezaji bei mbaya wa Klabu ya Tottenham Hotspur FC, Mkenya Victor Wanyama kwa ajili ya matembezi na mapumziko, ambapo mchezaji huyo atagharamia kila kitu.
Katika safari hiyo, amealikwa pia msanii wa Bongo Fleva, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ ambaye anatarajia kuongozana naye.
AISAPOTI TAIFA STARS
Wakati Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ikijiandaa katika mechi yake na Timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’, Pierre alionekana kushiriki katika kuhamasisha timu hiyo kushinda na kupata tiketi ya kushiriki katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon).
Alishiriki katika tangazo lililomwonesha akiwa uwanjani, amevaa jezi akiwa na mpira, akionesha jinsi timu ya Taifa Stars ilivyo kileleni. Hata katika siku ya mechi, Pierre alionekana kuwa mstari wa mbele
kuhamasisha Watanzania kuishangilia kwa nguvu Stars ambayo mwisho wa mchezo ilifanikiwa kuwachapa The Cranes bao 3-0.
Kwa ushindi huo, Stars itashiriki katika Fainali za Afcon baadaye mwezi Juni, mwaka huu nchini Misri ambapo nchi nyingine za Afrika Mashariki zilizofuzu ni pamoja na Uganda, Burundi na Kenya.
AWASHIKA VIONGOZI
Pierre ameonekana kuwashika viongozi mbalimbali wa Serikali kutokana na aina yake ya komedi isiyo rasmi. Katika siku ambayo Stars waliitwa Ikulu jijini Dar kupongezwa na Rais Dk John Pombe Magufuli kutokana na ushindi huo, katika hotuba yake, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alipongeza juhudi za wachezaji wa Stars na wahamasishaji akiwemo Pierre.
Mama Samia alisema: “Mheshimiwa Rais, nami niungane na wasemaji wengine, kuwashukuru wote walioleta ushindi. Kuna yule maarufu, nani huyu, Liquid… naye kafanya vitu vyake. Kwa hiyo jana ilikuwa furaha tupu, hongereni sana Kamati ya Hamasa.”
Mbali na Mama Samia, viongozi wengine walioonesha kumkubali Pierre ni pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla, Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule ‘Profesa Jay’, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Urban Mwegelo.
Jokate alikwenda mbali zaidi na kumwalika Pierre kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya wasichana wilayani Kisarawe aliyoipa jina la Tokomeza Zero Kisarawe, iliyofanyika wikiendi iliyopita katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar.
Kabla ya hafla hiyo, Pierre aliitangaza sana kupitia mitandao ya kijamii na hata aliposhiriki, alitoa mchango wake wa shilingi 100,000 kusapoti elimu Kisarawe. DC Jokate, katika kuonesha amethamini mchango wake, alitumia ukurasa wake wa Instagram kumshukuru Pierre, pia kumkaribisha Kisarawe aliposema kuna fusra ya biashara na zaidi aliahidi kumpa tenda ya utengenezaji wa madawati, kwa vile Pierre hujishughulisha na utengenezaji wa fenicha.
PIERRE LIQUID NI NANI?
Anaitwa Peter Gumbo, mfanyabiashara anayedili na utengenezaji wa fenicha eneo la Keko jijini Dar. Amepata umaarufu baada ya kuanza kuonekana kwa ‘clips’ zake mitandaoni akifanya vituko vya kilevi. Misemo yake maarufu kama “mama nakufaa”, “it’s ok”, “nitabaki kuwa juu, nitabaki kileleni” na mingine ndiyo imemfanya ajulikane na kupata umaarufu.
Televisheni za mtandaoni zimechangia kwa kiasi kikubwa kumtangaza Pierre ambaye kwa sasa anatambulika kama msanii ingawa hayupo kwenye kundi lolote la sanaa. Kutokana na vituko vyake, mbali na mialiko inayoonekana kumkalia vizuri, amepewa ubalozi wa bidhaa mbalimbali, jambo linalomwongezea kipato kutokana na ubunifu wake huo.