MJASIRIAMALI, mhamasishaji na mmiliki wa makampuni ya Global Group, Eric Shigongo, amewaasa wanawake nchini kuamini na kutumia vipaji walivyo navyo kwani vitawaletea mafanikio makubwa na kwamba wasikubali kukatishwa tamaa katika harakati za kuyatafuta mafanikio hayo.
Shigongo ameyasema hayo Jumamosi, Aprili 6, 2019, wakati akitoa neno la nasaha katika kilele cha Tuzo za Malkia wa Nguvu zilizoandaliwa na Clouds Media na kufanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mhamasishaji huyo mashuhuri nchini amewaeleza kinamama hao kuwa kila binadamu ana nafasi yake ya kufanikiwa na kwamba kinachotakiwa ni kujiamini na kuukataa mfumo unaowagandamiza wanawake na kuwanyima fursa ya kufanya maamuzi yao kwa uhuru.
“Naomba mnisikilize kwa makini, mwanamke uliyepo hapa leo na unayenisikiliza, una uwezo wa kufanya jambo kubwa na ukaacha alama siku ukiondoka duniani. Usisikilize watu wanachosema kuhusu wewe, ni Mungu tu aliyekuumba na kukupulizia uhai ndiye anafahamu makusudi ya kukuleta duniani.
“Amini kwamba unaweza kufanya jambo leo likabadili maisha yako na kukuondoa katika umasikini. Mimi niliitwa maskini na mjinga, nikaamini kwamba ni mjinga kweli, nikafeli darasa la saba. Sikwenda sekondari, lakini leo hii aliyeitwa mjinga ndiye ameshika hapa maiki. Ningeaamini maneno yao nisingekuwa Shigongo mnayeniona hapa,” alisisitiza.