×

Yatima Muuza Maji Aliyewajengea Vikongwe Masikini Nyumba! – Video


KIJANA mmoja mkazi wa Kijiji cha Twabagondozi wilayani Kibondo mkoani Kigoma, ameonyesha kuwa si lazima kuwa na pesa nyingi ili kuweza kusaidia watu wengine wenye mahitaji baada ya kujitolea kuwasaidia wazee wasiojiweza 15 katika kijiji chao kwa kuwajengea nyumba za kuishi.

 

Tito Mitagato ambaye ni yatima, shughuli yake kuu ni kuuza maji kwa kutumia baiskeli lakini licha ya kipato kidogo anachokipata hiyo haikumzuia kutimiza ndoto yake ya kuwasaidia wazee kwani hiyo imekuwa ni ndoto yake ya muda mrefu tangu akiwa mdogo.

 

Amesema ndoto hiyo ilikuja baada ya yeye kupitia katika hali ngumu ya maisha ya kulelewa na bibi yake baada ya baba yake kufariki dunia na baadaye mama yake kumuacha kwa bibi yake baada ya kuolewa na mume mwingine.

 

Tito mwenye mke, amesema hununua vifaa vya ujenzi na kujenga yeye mwenyewe ambapo ameeleza namna anavyoweza kugawa muda wake kwa ajili ya majukumu ya kifamilia na muda wa kuwasaidia wazee hao.

 

Mmoja wa wazee aliowasaidia ni Maria Kafugu, anasema kijana huyo ana roho ya pekee kwani licha ya kuwa na watoto wake hawajafanya kitu kama alichokifanya Tito.

 

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Twabagondozi, wakiwemo vijana wenzake wamemuelezea kijana huyo kama mfano wa kuigwa na wengine, huku wakiiomba serikali imtumie kama balozi wa kusaidia watu wenye mahitaji.

 

Kwa mujibu wa kijana huyo (Tito), bado anatamani kusaidia watu wengi zaidi kwani wahitaji ni wengi lakini hali ya kipato chake humkwamisha kutimiza azma yake hiyo.

TAZAMA TUKIO HILO HAPA