
UONGOZI wa Simba chini ya Bodi ya Wakurugenzi, umefanya kikao kujadili kama wamuongezee mkataba kocha wao mpya, Mbelgiji, Patrick Aussems au wampotezee. Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo itoke kufungwa na TP Mazembe mabao 4-1 katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mkataba wa kocha huyo na Simba unamalizika mwishoni mwa msimu huu ambapo Julai, mwaka jana alijiunga na timu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano ni kwamba bado kuna hatihati kutokana na maazimio ya kikao cha bodi ya viongozi wa timu hiyo chini ya mwekezaji wake, bilionea, Mohammed Dewji.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa katika kikao hicho kilichokaa juzi usiku katika Hoteli ya Serena, viongozi hao baadhi wameonesha kutoridhishwa na uwezo wake katika michuano ya kimataifa kila wanapocheza ugenini, lakini suala hilo likabaki kwa mwekezaji kufanya maamuzi ya mwisho.
“Tushukuru kwa hatua ambayo timu imefikia katika michuano ya kimataifa kwa kufanikiwa kufika robo fainali. “Kama viongozi tumepongeza sana kocha kutokana na hatua hiyo, lakini kulikuwa na baadhi ya wachache wanahoji kama tumuongezee mkataba au la lakini tumeona hilo tuliache kwanza kwa sasa kwa kuwa tupo kwenye ligi,”alisema mtoa taarifa huyo.
Championi lilipopata taarifa hiyo lilimtafuta Katibu wa timu hiyo, Anold Kashembe ambapo
alisema: “Kwa sasa hatuwezi kujadili masuala ya mkataba kwa kuwa bado tupo kwenye ligi, lakini ni kweli kuwa jana tulikuwa na kikao na kumpongeza kocha na wengine kwa hatua ambayo tulifikia kwenye michuano ya kimataifa. “Tageti yetu ilikuwa kufika hatua ya makundi lakini tukavuka hadi robo, kuna makosa tumeyaona, likiwemo suala la kushinda nyumbani na kufungwa ugenini, nafikiri tutarekebisha msimu ujao yasijirudie.
Stori na Wilbert Molandi, Dar es Salaam