
KATIKA kuhakikisha timu yake inauchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya pili mfululizo, Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, ameahidi kupata ushindi katika michezo 15 iliyosalia kumaliza msimu huu wa 2018/19 katika ligi hiyo.
Kauli hiyo aliitoa juzi Jumatano mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga ambapo ulimalizika kwa Simba kushinda mabao 2-1 yote yakifungwa na Meddie Kagere.
Simba inatarajiwa kujitupa tena kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, kesho Jumamosi kuvaana na Kagera Sugar mchezo unaotarajiwa kuwa na upinzani mkubwa.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Aussems alisema amejiandaa kukabiliana na upinzani kutoka kwa wapinzani wake atakaokutana nao katika michezo hiyo ijayo ya ligi. Kauli ya kushinda mechi zote 15 zilizosalia inamaanisha anataka kuona wakimaliza wakiwa na pointi 105 kwa kuwa sasa wana pointi 60.
Aussems amesema kikubwa anataka kutimiza malengo aliyojiwekea ya kuhakikisha anauchukua ubingwa wa ligi ili msimu ujao ashiriki tena Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa ni baada ya kupata uzoefu na kujifunza changamoto mbalimbali.
“Haikuwa rahisi kupata ushindi kwenye mchezo wetu na Coastal Union kutokana na hali ya uwanja tuliyokutana nayo Tanga, lakini vijana wangu walipambana na kufanikiwa kuvuna pointi tatu. “Katika mchezo huo tulifanikiwa kumiliki mchezo na mabadiliko ambayo niliyafanya yakatusaidia kupata mabao na mwisho wa mchezo tukapata pointi tatu muhimu.
“Nimezungumza na vijana wangu na kuwaambia kuwa ninataka kuona timu inapata matokeo mazuri katika michezo yote tuliyoibakiza ya ligi kwa kuchukua pointi tatu. “Ninafahamu siyo kazi rahisi, lakini nimewasisitiza vijana wangu kushika maelekezo yangu na kuyafanyia kazi kwenye mechi na lengo ni kuchukua pointi tatu,” alisema Aussems.
Stori na Wilbert Molandi