WATU wengi wamejikuta wakisherehekea Sikukuu ya Pasaka pasipo kujua wanachokisherehekea; wengine ukiwauliza Pasaka ni nini, hawana majibu. Wengine watakujibu kwamba hiyo ni sikukuu tu, kama sikukuu zingine.
Nifafanue tu kwamba Pasaka ni jina la sadaka kabla halijawa jina la sikukuu. Pasaka ni sherehe ya Kiyahudi iliyowakumbusha jinsi Mungu alivyowakomboa Waisraeli kutoka katika utumwa wa Misri mwaka wa 1513 K.W.K.
Neno ‘pasaka’ linarejelea kipindi ambacho Mungu aliwalinda Waisraeli kutokana na lile pigo kubwa la kuuawa kwa kila mzaliwa wa kwanza wa Misri (Kutoka 12:27; 13:15).
Kabla ya Mungu kuanza kutekeleza pigo hilo, aliwaambia Waisraeli wapake damu ya mwanakondoo au mbuzi kwenye milango yao.
Mungu angetuma malaika mtoa roho na angeona ishara hiyo na ‘kupita juu’ ya nyumba zao na hivyo wazaliwa wao wa kwanza wasingeuawa (Kutoka 12: 7, 13).
Jambo hili lilikuwa agizo la Mungu kwao ili atumie kitendo hicho kuwafungua toka kwenye utumwa wa miaka 430 wakiwa mikononi mwa Wamisri.
Ukisoma katika Biblia Takatifu, kitabu cha Kutoka 12: 11, 44 anazungumza juu ya kumla pasaka akiwa na maana ya kumla mwanakondoo aliyetolewa sadaka siku hiyo.
Katika kitabu cha Kutoka 12:27, huyo mwanakondoo anajulikana kama dhabihu ya Pasaka ya Bwana.
Mungu aliwapa agizo la kuwa na kumbukumbu ya jambo hilo kila mwaka katika vizazi vyao vyote.
Ni rahisi sana kupoteza maana ya Pasaka, kama msisitizo wa Wakristo utakuwa kwenye sikukuu iitwayo Pasaka, badala ya kuweka msisitizo kwenye sadaka iitwayo pasaka.
Msisitizo wa jambo hili tunauona tunaposoma ya kwamba Yesu Kristo ni Pasaka wetu! Yaani ni aina ya sadaka iitwayo pasaka kwetu, ili Mungu aitumie damu yake kutuokoa.
“….kwa maana Pasaka wetu amekwishakutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo.” (1Wakorintho 5:7).
Mungu alipomtoa Yesu Kristo kama Pasaka wetu, yaani sadaka iitwayo pasaka, kati ya jambo kubwa lililofanyika lilikuwa ni kukombolewa kwa mwanadamu kutoka katika umauti yaani nguvu za giza na kuingizwa kwenye ufalme wa Mungu yaani uzima wa milele.
Unaposoma kitabu cha Wakolosai 1:13,14 neno la Mungu linasema hivi: “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa mwana wa pendo lake; 14 ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi.”
Kitabu cha 1Yohana 3:14 kinasisitiza hilo kwa kuandika: “Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti.”
Faida walizopata wana wa Israeli kwa kutoa sadaka ya mwanakondoo aliyeitwa Pasaka, unaweza ukazipata na wewe kwa kupitia kifo cha Yesu msalabani kama sadaka ya pasaka kwa ajili yetu.
Kama tulivyoona hapo juu, Waisraeli waliokolewa na damu ya mnyama waliyoipaka katika miimo na miisho ya milango yao na ndipo malaika wa Bwana alipotambua na kupita juu, lakini Wakristo tunaambiwa Pasaka wetu ni Yesu mwenyewe aliyetuokoa kwa damu yake.
Tunasoma katika Yohana 1:36 “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwanakondoo asiye na hila, asiye na waa, yaani ya Kristo.”
Basi kama tulivyoona neno la Mungu linatuthibitishia ya kuwa kwa sasa Wakristo tunaokolewa na damu ya Yesu ambaye ndiye Pasaka wetu na si kwa damu ya mnyama aliyekuwa pasaka kwa watu wa kale.
Ni kazi yako kujua na kufuatilia ni vitu gani wana wa Israeli walifaidika ili na wewe imani yako ijengeke na uweze kuviomba kwa Mungu ili akupe na wewe katika Kristo Yesu , aliye Pasaka kwetu.
Kumbuka kuangalia Pasaka kwa jicho la sadaka ya Yesu pale msalabani, ndipo hata sikukuu itakuwa muhimu kwako kiroho.
WAJALI WAHITAJI
Lakini unaweza kwenda mbali zaidi kwa kutoa sadaka yako kwa wahitaji. Angalia kwenye jamii yako, wale wenye changamoto, wasaidie waweze kusherehekea nao Pasaka japo kwa chakula, vinywaji na mavazi.
Hujachelewa, ingawa kesho ndiyo Pasaka yenyewe, lakini kwa kujua ukweli huu leo, unaweza kufanya kitu fulani kwa ajili ya watu wako wa karibu.
Jitafakari; umewakumbuka wazazi wako, ndugu zako, familia yako au jirani zako wanaohitaji? Mungu akupe moyo wa kuelewa maana ya Pasaka na kujitoa kwa sadaka ili kuikamilisha.
MAKALA: Elvan Stambuli