
Rais Mstaafu wa Tanzania wa awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amekwenda kuhani msiba nyumbani kwa marehemu Dkt. Reginald Mengi, Kinondoni Hananasif jijini Dar es Salaam.
Kikwete alitumia muda huo kuwapa pole ndugu, jamaa na marafiki kufuatia msiba huo mzito na amewataka Watanzania watulie na kutojichanganya na maneno yanayosambazwa katika mitandao ya kijami kuhusiana na sababu za kifo cha Mengi kilichotokea Mei 2 huko Dubai.
Aliwaomba Watanzania kutulia hadi binti yake na mdogo wake marehemu Mengi, Benjain, waliokuwa naye huko Dubai watakaporejea nchini kwani alisema wataeleza chanzo cha kifo chake.
“Nimepoteza kaka na rafiki, mzee Mengi alikuwa mtu wa aina yake, ni wachache sana duniani……. Tuache uongo, tuache kuingiza yasiyokuwepo, kama kweli tunampenda Dkt. Mengi basi haya mengine ya uongouongo, hadithi za kutunga hizi tungeachana nazo.

”Sisi wengine tuendelee kuwa watulivu, tuache kuingiza yasiyokuwepo tukaichanganya jamii, tusubiri ukweli, ukweli tutaupata. Alifariki Dubai mdogo wake Benjaini alikuwepo binti yake alikuwepo, hao ndio wana ukweli. Hayo mengine mnayosomasoma nadhani kwa sasa yaacheni tusibiri wakirudi hao nadhani watatuambia ni nini hasa kilitokea na ilikuaje mpaka kifo kikamtokea,” amesema Kikwete.
Mbali na hilo Kikwete ameomba mazuri ya Mengi yaendelee kudumishwa kwani alikuwa ni msaada wa watu wengi na kwa nafasi yake ametimiza kusudi lake la kuishi duniani kwani utajiri wake aliweza kuutumia vizuri na kuwa daraja la mafanikio kwa watu wengi.
Aidha, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro amesema anafuatilia yanayoendelea katika mitandao ya kijamii na hawatayapuuza, wanafuatilia kuona kama kuna mkono wa mtu umehusika kifo cha Mengi na ikiwa hivyo sheria itachukua mkondo wake kwani yapo mengi yaliyoelezwa kwenye mitandao ya kijamii.