The House of Favourite Newspapers

MOYO WA SHUKRANI UNA MAANA KWENYE MAPENZI !-2

NI Juma­mosi ny­ingine tena tunakutana kwenye ukurasa wetu wa kuzun­gumzia mambo mapenzi na uhusiano kwa jumla. Naamini mengi unajifunza kupitia kona hii.  Ndugu zangu, kiukweli hapa ni mahali sahihi kabisa pa kupanuana mawazo kuhusu maisha na mapenzi. Ukiwa mdau wa ukurasa huu utaendelea kuimarisha uhusiano wako siku hadi siku. Napokea pongezi zenu wasomaji mlizonitumia baada ya makala ya utangulizi wiki iliyopita. Ilikuwa ni sehemu ya kwanza na leo tunamalizia sehemu ya mwisho ya somo letu.

Naahidi kuboresha zaidi ili mpate kitu kizuri zaidi na uhusiano uwe wenye afya na amani kwa wenzi wenu. Au siyo jamani? Naamini tunakwenda sawa. Marafiki zangu, wiki iliyopita nilianza kwa kueleza tofauti iliyopo kati ya urafiki au uchumba na ndoa. Mapenzi yale ya urafiki ni tofauti kabisa na kuwa ndani ya ndoa. Kwenye uchumba kuna mambo ya kufurahisha zaidi, lengo kuu huwa kupeana raha na starehe za hapa na pale.

Lakini sasa mnapoingia kwenye ndoa, mapenzi yapo tena yanakuwa na nguvu zaidi lakini kuna vitu kidogo vinabadilika. Hata kama ukiona mwenzako kuna vitu hakufanyii, usikasirike, angalia yale ya msingi zaidi kama anakupatia. Si rahisi akakupa kila kitu, ridhika naye kwa kuwa moyoni umewekeza upendo wako. Vipengele vifuatavyo, vinafafanua zaidi.

HAKUNA RUFAA

Kwanza kabisa unatakiwa kufahamu kwamba, hakuna rufaa katika ndoa. Ukishaingia umeingia. Ni vizuri kuwa mtulivu na kuangalia zaidi mambo ya msingi. Achana na fikra mbaya kwa mwenzako, wekeza upendo wako kwake. Mwamini na ishi naye kwa akili huku ukijaribu kumshauri mambo mbalimbali ya maisha yenu.

FURAHA YA NDOA

Yapo mambo mengi ya muhimu kwenye ndoa, lakini jambo kubwa na la msingi zaidi ni pamoja na tendo la ndoa. Lazima wanandoa wawe na uhakika wa kupata tendo la ndoa. Tendo lenyewe linatakiwa kufanyika vizuri na kwa usahihi. Siyo harakaharaka bila ubunifu. Kufanya hivyo ni kuacha mianya ya mmoja wenu kufikiria kutoka nje ya ndoa.

FAMILIA

Majukumu ya familia ni kati ya mambo yanayozidisha furaha ya ndoa. Kama wanandoa wanakuwa makini kuhakikisha familia inakuwa yenye furaha ni jambo zuri. Lazima watoto wapatiwe elimu bora, uhakika wa lishe, malazi na mambo mengine kama hayo bila kusahau malezi mazuri ya kiimani. Ukishindwa kufuatilia hayo kwa kina, mapenzi yenu hayatakuwa na maana.

MIPANGO YA BAADAYE

Maisha ni mipango, hamuwezi kufikiria starehe tena kama ilivyokuwa kwenye uchumba. Kwenye muunganiko wa ndoa kuna suala la maendeleo na mipango ya baadaye. Hapo mnatakiwa kuwaweka watoto wenu mbele, maana lazima wawe na akiba yao ambayo mtawaachia. Lazima mfikirie kuhusu rasilimali kwa ajili yao.

KUJALIANA

Kila mmoja anaweza kukutana na changamoto kwa wakati wake. Kuna suala la matatizo kazini au msongo wa mawazo. Majukumu ya familia ya upande mmoja au ndugu wa mwenzako.

Mambo kama hayo mkishirikiana kuyatatua huongeza mapenzi ya dhati. Kwa mfano, mmoja wenu anaweza kuugua. Ni jambo zuri sasa kuwa karibu naye na kumpa furaha ili ajione yupo na chaguo lililo kamili. Maisha ni zaidi ya starehe za kawaida. Majukumu ya familia ni muhimu zaidi kuliko yale mahaba ya mwanzo. Huu ni ukweli ambao wanandoa wengi (hasa wanawake) wanaukimbia.

Wiki ijayo nitakuwa hapa na mada nyingine, USIKOSE!

Comments are closed.