The House of Favourite Newspapers

USIJIENDEKEZE, USIPOANGALIA UTAKUFA BURE KWA WIVU

ASSALAM Alaikum! Ni furaha yangu kwa mara nyingine tena kukutana nawe kwenye safu yetu hii ya Love Zone. Tumshukuru Muumba wetu kwa kutujaalia uhai na afya njema, lakini zaidi ya hapo tumshukuru pia kwa kutuumbia kitu mapenzi.  Siku zote hatutaacha kuzungumza juu ya mapenzi kwani ni ukweli usiopingika kwamba mapenzi ndio maisha yetu. Tunafanya kazi usiku na mchana, tunahangaika huku na huko, lakini mwisho wa siku tunafikiria jinsi gani tutaboresha na kufurahia maisha na wapenzi wetu. Tunafikiria pia ni jinsi gani tunaweza tukapata utulivu na amani katika maisha ya kimapenzi na wapenzi wetu, waume zetu au wake zetu katika siku zote za maisha yetu.

Wiki hii nimeona ni vyema tukabadili-shana uzoefu juu ya suala zima la wivu katika mapenzi. Mtakubaliana nami kuwa suala la kuwa na wivu kwa mpenzi wako ni jambo lisilokwepeka hasa kwa sababu kubwa ya kuaminika kwake kwamba kuwa na wivu ni moja ya kigezo cha kuonesha ni jinsi gani unampenda mpenzio na kwamba hauko tayari kwa namna yoyote ile kushea na mwingine, ndio maana wanawake wengi hawataki kusikia suala la ukewenza kabisaa! Hata kama jambo hilo limepewa baraka zote na dini au tamaduni zao.

Lakini kubwa katika wivu ni ile kutokuwa tayari kuona tunasalitiwa na wapenzi na hasa kwa wale tunaowapenda ukweli toka moyoni mwetu na zaidi ukute ndo tumeshawa-gharamikia kiasi cha kutosha na kujitoa kwao kwa kila kitu!

Umeshawahi kusikia kauli kama ‘Jamani mke (au mume) anauma! Au kauli kama mke wa mtu sumu” na hugeuka sumu kweli pale unapobambwa na mali za wenyewe, kufanyiwa kitu mbaya inakuwa sio jambo la ajabu sana. Nikuambie tu kwamba, mapenzi ni full uchoyo, ni full kujipendelea! Mpenzi wanaume kwa mfano, anaweza kufikiria kwamba ni yeye tu ndiye anayestahili na anayeweza kumfanya mpenzi wake acheke na kufurahi.

Na kwamba akitokea mwanaume mwingine akapata nafasi ya kumfurahisha mpenzi huyo hata katika stori za kawaida tu, unaweza ukasikia akisema, ‘Hivi wewe mna nini na huyo jamaa, mbona unamchekea chekea hivyo, au…!’ Hiyo ndiyo choyo ya penzi na kikubwa kinachofanyika hapo ni ile tu kujaribu kulinda maslahi binafsi.

Pamoja na ukweli kwamba tabia ya wivu inapozidi hugeuka kuwa kero, lakini kabla hatujafika huko hebu tuangalie nafasi ya wivu katika mapenzi yetu. Yaani swali ni kwamba, je! Wivu katika mapenzi unaleta maana? Nionavyo mimi wivu ukitumika vizuri unaleta maana na una nafasi muhimu sana katika mapenzi kwa sababu zifuatazo:

Kwanza huonesha kujali. Sote tunaamini pasipo na wivu hata chembe, hapana mapenzi ya kweli. Kumuonesha wivu mpenzi wako ni kumjulisha ni kiasi gani unamjali na kumpenda na kwamba yeye ni mtu maalum sana kwako. Pili, wivu unaonesha kuthamini uhusiano. Kwa mfano unaweza kumsikia mtu akisema;

“Sio kama sikuamini dear, bali wivu wangu kwako ni katika kuuthamini uhusiano wetu, mimi na wewe ni umoja wenye thamani kubwa, tusiruhusu kuuchezea nje yetu! Huu ni mfano wa ujumbe unaoonesha maana na nafasi ya wivu katika mahusiano ya kimapenzi. Tatu, wivu unaleta mazingira ya kujijengea heshima. Kwa mfano mume mwenye wivu na mkewe hujijengea heshima ya kwamba kweli anamjali na kumpenda mkewe lakini pia anaweka mazingira ya kutosumbuliwa kwa mke wake huyo.

MWANDISHI:

Amran Kaima

Maoni/Ushauri 0658 798787

Comments are closed.