
MWANADADA wa Kitanzania, Angel Eaton, kwa mara ya kwanza amezungumza kuhusu magumu aliyopitia mpaka kutoboa na kufanikisha kunyakua jumla ya tuzo na makombe 34 ya mchezo wa GOLF ikiwemo tuzo ya hivi karibuni ya Ubingwa wa GOLF Afrika Mashariki na Kati ya mwaka 2019.

Angel ambaye kituo chake cha michezo kipo Lugalo jijini Dar es Salaam amefunguka hayo wakati akifanya kipindi maalum na Kituo cha 255 Global Radio, leo Jumanne, Mei 21, 2019 alipotembelea studio za radio hiyo.

“Nikiwa mdogo nilianza kucheza tennis na GOLF taratibu sana, mara ya kwanza sikuupenda kabisa huu mchezo, lakini nilipondelea nilijikuta nikizoea, nikaona kipaji changu hakipo kwenye tennis, hivyo nikahamia rasmi kwenye GOLF.

“Ili uweze kuumudu mchezo huo, kuna stages tatu, kwa wanawake huwa tunaanzia na hand cape 36, lakini wanaume wanaanzia hand cape 24, utaingia 18, kisha 12 na mwisho 0, baada ya hapo unakuwa professional.

“Kufikia stages hizi zote kwangu mimi ilichukua mwaka mzima kuuelewa vizuri mchezo, na hapo sio kupiga mipira kumi, unatakiwa angalau upige mipira 500 kwa siku, kwa hiyo haikuwa kazi rahisi,” alisema.

Amesema kwa sasa ana tuzo zipatazo 34 ambazo ameshinda katika mashindano mbalimbali ya kimataifa na ya ndani ikiwemo ya Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati aliyopata hivi karibuni huku akitaja kuwa siri ya mafanikio yake hayo ni kujituma katika mazoezi yake na kuondoa uoga.

Aidha, gazeti namba moja la michezo Tanzania, Championi linalochapishwa na Kampuni ya Global Publishers limemtunuku Angel, Tuzo ya Heshima kutokana na umahiri wake kwenye tasnia ya GOLF na kutambua mchango wake kwenye mchezo huo na namna anavyoiwakilisha nchi yetu kimataifa.

Akifungukia tuzo hiyo, Angel amesema: “Kwa kweli ni jambo kubwa sana katika maisha yangu ambalo Championi wamenifanyia leo, sijawahi kufanyiwa kitu kama hiki, sikuwahi kufikiria kama kitu hiki ningeweza kufanyiwa.

“Ninawashukuru sana Global Publishers na Global Radio kwa kutambua mchango wangu, hii imenipa hamasa kubwa na nguvu ya kuendelea kupambana zaidi, sasa ninajiona kama staa.”

…Akiwa katika mahojiano.
Amesema iwapo akipata nafasi katika mashindano y Olympic ya mwakani yupo tayari kwenda kuiwakilisha nchi vizuri na anaamini kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusakata GOLF, na sapoti ya Watanzania, atanyakua ushindi na kuipaisha Tanzania tena.

Akizungumzia changamoto katika mchezo huo, Angel amedai kuwa tatizo kubwa ni ubovu wa viwanja, miundombinu ya mchezo huo, vifaa vya michezo ambavyo ni bei ghali sana (set moja inagharimu zaidi ya Tsh milioni 3) hivyo watu wengi hushindwa kumudu kuvinunua.

Amebainisha jambo jingine linalokwamisha ukuaji wa mchezo huo hapa nchini ni ugumu wa kupata wadhamini.

Angel Eaton
Historia fupi
JINA la Angel Eaton, si geni masikioni mwa wadau mbalimbali wa michezo ndani na nje ya Bara la Afrika Mashariki na Kati, umaarufu wake umetokana na kazi nzuri anazofanya uwanjani, katika safari ya kuiwakilisha vyema klabu yake ya Lugalo na Tanzania kwa ujumla.

Mwanadada huyu alizaliwa mwaka 1990 katika hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam, anatokea katika kabila la Wamakonde lakini pia, ni mama wa mtoto mmoja wa kike anayefahamika kwa jina la Delight.

Mwaka 2006, ulikuwa mwanzo wake wa kujifunza mchezo wa gofu akiwa katika klabu ya Gymkhana jijini hapa kabla ya 2014 kuhamishia virago vyake katika klabu ya Lugalo, anayoitumikia hadi sasa.

Mashindano aliyochukuwa ubingwa
2006– Aliwahi kushinda kupitia mashindano ya ‘Tanzania Ladies open’ (Overall Winner), na mengine mengi ya ndani na nje ya nchi.

2007– Alishinda mashindano ya Mwalimu Julies Nyerere (Overall Winner)
-CDF Cup
-Uganda Ladies Open
-Dar Gymkhana Trophy nakadhalika

2008– Lady Cameroon Cup
-Uganda Ladies Open
-Tanzania Ladies Open
-Leisure Ladies Open
-Toyota Golf Cup, nakadhalika

2010– Zambia ladies Open
-Uganda Ladies Open, n kadhalika

2011- Mombasa Ladies Open
-Kenya Ladies Open
-Uganda Ladies Open
-Morogoro Ladies Open
-Tanzania Ladies Open, nakadhalika

2012– Uganda Ladies Open
-Tanzania Ladies Open, nakadhalika.

2016– Uganda Ladies Open
-Nairobi Ladies Open, nakadhalika

2018– aliibuka kidedea nchini Nigeria

2019– aliibuka bingwa wa mashindano ya wanawake nchini Malawi
