×

Algeria Mabingwa wa Afcon 2019, Yaifunga Senegal Bao 1-0

ALGERIA usiku wa kuamkia leo wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa Afrika baada ya kuwachapa Senegal bao 1-0 kwenye Dimba la Cairo nchini Misri. Senegal kwa mara ya kwanza walionyesha udhaifu kwenye safu ya ulinzi baada ya kumkosa beki wake mahiri, Kalidou Koulibaly ambaye alikuwa na kadi mbili za njano.

Tangu michuano hii ianze, Senegal walikuwa wameruhusu kufungwa bao moja tu na ndiyo timu iliyokuwa imeruhusu mabao machache kabla ya fainali. Kwa upande wa Algeria, imemaliza michuano ikiwa imeruhusu mabao mawili pekee, huku ikiwa haijapoteza hata mchezo mmoja. Algeria walijipatia bao hilo katika dakika ya pili tu ya mchezo lililofungwa na Bagdad Bounebdjah, baada ya kupiga shuti kali ambalo lilimgonga beki wa Senegal, Cheikhou Kouyate na kujaa wavuni.

Hata hivyo, baada ya bao hilo, Senegal walionekana kuamka na kuanza kuliandama lango la Algeria huku staa wao Sadio Mane akipambana kwa nguvu kubwa kutafuta bao.

 

Dakika 45 za kwanza zilimaliza kwa timu zote kupiga shuti mojamoja langoni, huku Senegal wakitawala kwa kupiga pasi 157 na Algeria ambao walirudi nyuma baada ya kupata bao, wakipiga pasi 98 tu.

Katika dakika ya 60 ya mchezo, mwamuzi aliwapa Senegal mkwaju wa penalti baada ya beki mmoja wa Algeria kuunawa mpira, lakini alipokwenda kuangalia kwenye VAR alibadilisha mawazo.

 

Kipindi cha pili Senegal walionyesha kiwango cha juu baada ya kupiga mashuti makali langoni mwa Algeria lakini mara kwa mara washambuliaji wao walikosa umakini.

Hii ni mara ya pili, Algeria wanatwaa ubingwa huu baada ya mara ya kwanza kuutwaa mwaka 1990. Kwa upande wa Senegal, hii ilikuwa mara yao ya pili kufi ka fainali ya michuano hii na kuliona kombe likienda nchi nyingine baada ya kizazi chao cha dhahabu kufi ka fainali mwaka 2012, na kushindwa tena kutwaa ubingwa.

Baghdad Bounedjah baada ya kufunga dakika ya pili kipindi cha kwanza.

Senegal walimaliza dakika tisini wakiwa wamepiga jumla ya mashuti 11, Algeria walipiga moja, walipiga pasi 320 Algeria walipiga 201, kona Senegal walipiga sita Algeria 2.