
TIMU ya Yanga itacheza dhidi ya Kariobangi Sharks ya Kenya katika kilele cha Wiki ya Mwananchi Agosti 4, kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Akizungumza Katibu Mkuu wa Hamasa wa klabu hiyo, Deo Muta amesema mchezo huo utakuwa katika viingilio vitatu ambapo kiingilio cha chini ni Sh 5,000 kwa mzunguko wa orange.
Muta alisema kwa upande wa VIP B kiingilio kitakuwa Sh 30000 wakati VIP A itakuwa ni Sh 100,000.

Yanga ilikuwa imepanga kucheza na AS Vita ya DR Congo ambao wameshindwa kuja nchini kutokana na kubanwa na ratiba ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela amesema Julai 27 mwaka huu wanatarajia kufanya uzinduzi rasmi wa tamasha hilo makao makuu ya klabu hiyo.
“Uzinduzi tunatarajia kuufanyia klabuni kwa kuanza na kufanya usafi na baadae tunaenda katika viwanja vya Mwembeyanga ambapo watakuwa na mechi ya timu ya vijana na mashabiki wa timu hiyo,” alisema.
“Kikosi chetu kuelekea mchezo huo kipo imara na kimejiandaa vyema kuhakikisha kinatoa burudani kwa mashabiki zake ambao wanahamu ya kuwaona.”
“Tuna kikosi kipana tumesajili kwaajili ya mashindano ya ndani na kimataifa lengo ni kuirudisha timu yetu kwenye ushindani kama misimu mitatu iliyopita,” alisema Mwakalebela.