×

Balinya, Sibomana Wafunika Mastaa wote Simba SC

HALI ya mambo ndani ya vikosi vya Simba na Yanga ni moto, hivyo ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mazoezi kabambe ambayo timu hizo kwa sasa zinayafanya kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.

 

Kwa sasa Simba ipo nchini Afrika Kusini ikijiandaa na michuano hiyo wakati Yanga yenyewe imejichimbia mkoani Morogoro ambako inapiga tizi la nguvu.

 

Mpaka sasa timu hizo zikiwa katika kambi hizo, zimefanikiwa kucheza mechi mbalimbali za kirafiki kwa ajili ya kuwasaidia viongozi wa mabenchi ya ufundi kuona uwezo wa wachezaji wao wapya waliowasajili hivi karibuni na zaidi ni wale wa safu za ushambuliaji.

Simba yenyewe mpaka sasa imecheza mechi mbili za kirafiki wakati Yanga imecheza mechi tatu. Hata hivyo katika mechi hizo wachezaji wapya wa safu ya ushambuliaji ya Yanga wanaonekana kuwafunika vilivyo wenzao wa Simba.

 

Washambuliaji hao wa Yanga wakiongozwa na Mnyarwanda, Patrick Sibomana wamewafunika wenzao wa Simba kutokana na kufunga mabao mengi ambapo mpaka sasa wamefanikiwa kufunga mabao 10.

Katika mechi hizo, Sibomana amefanikiwa kufunga manne wakati Mganda, Juma Balinya yeye kafunga matatu. Wangine waliofunga katika mechi hizo ni Mnamibia, Sadney Urikhob ambaye ana mabao mawili pamoja na Mnyarwanda Issa Bigirimana ambaye yeye ana bao moja.

 

Mzambia, Maybin Kalengo yeye hana bao lolote na hiyo inatokana na muda mwingi kuwa nje ya uwanja kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya mguu aliyoyapata mazoezini hivi karibuni, hivyo hajapata nafasi ya kuitumikia timu hiyo katika mechi hizo za kirafiki.

 

Kwa upande wa Simba, mshambuliaji wake Mbrazil,Wilker Henrique da Silva, ndiye anayeonekana kuwa moto kuliko wengine wote waliosajiliwa karibuni ambao ni pamoja na Mkongomani Deo Kanda, Mkenya Francis Kahata,

 

Ibrahim Ajibu pamoja na Miraji Athumani ‘Sheva’. Wilker peke yake kati ya washambuliaji hao ndiye ambaye anaonekana kuwa moto kwani katika mechi hizo mbili, amefunga bao moja huku wengine wakiwa hawana bao lolote. Kutokana na hali hiyo, washambuliaji wapya wa Yanga, wanaonekana kuwa moto ukilinganisha na wale wa Simba ambao kasi yao bado haijakuwa kubwa.

 

Hata hivyo, aina za mechi ni tofauti, pia aina ya kambi ni tofauti, kwa hiyo hukumu zaidi itapatikana katika mashindano halisi, hasa michuano ya kimataifa ambayo inaanza mapema mwezi ujao. Washambuliaji hao wa Simba kesho Jumamosi, watakuwa uwanjani kuonyesha makeke yao wakati watakapocheza mechi ya kirafiki na wapinzani wa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Township Rollers ya Botswana.

SWEETBERT LUKONGE NA SAID ALLY, Dar