
KITENDO cha wachezaji Ibrahim Ajibu na John Bocco kuwepo kwenye kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars iliyocheza na Kenya jana Jumapili, kimemchanganya vilivyo kocha wao wa Simba, Patrick Aussems.
Kocha huyo amedai kuwa wachezaji hao wataharibu mipango yake kwenye mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na muda ambao watakaokaa ndani ya kambi ya Stars.
Kocha huyo ameliambia Championi Jumatatu, kuwa wachezaji hao watarudi siku chache kabla ya mechi yao hiyo ya kimataifa ambapo wamepangwa kucheza na UD do Songo ya Msumbiji kati ya Agosti 9 hadi 11.

“Wachezaji hao ambao wameenda Stars, kwa namna fulani wametibua mipango yangu kwa sababu watarudi siku mbili kabla ya sisi kucheza na UD Songo.
“Wakija ni lazima wapewe mafunzo maalum ili wawe sawa na wenzao, kitu ambacho unaona kinatibua mbinu zangu,” alisema Aussems.
Aussems ataiongoza Simba kwenye michuano ya kimataifa kwa mara ya pili mfululizo ambapo kwa msimu huu watacheza na mabingwa wa Msumbiji UD do Songo. Mechi ya kwanza watacheza nchini Msumbiji Agosti 9-11 na watarudiana Dar es Salaam Agosti 23-25.