×

Polisi Singida Wakamata ‘Luteni Feki’ wa JWTZ

 

 

 

Image result for Kamanda wa Polisi Singida, Sweetbert Njewike

JESHI la Polisi  mkoani Singida limemkamata mkazi mmoja  wa jijini Arusha, Amieli Stephano (29), kwa tuhuma ya  kujifanya Ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),  mwenye cheo cha luteni. Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike, alisema mtuhumiwa alikamatwa Julai 17, mwaka huu saa 6 mchana katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa (Bomani) mjini hapa.

Alisema uchunguzi wa awali, unaonyesha mtuhumiwa alikuwa maeneo  ya Bomani kumwombea ndugu yake achaguliwe kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). “Kabla ya kuwasilisha ombi hilo, mtuhumiwa alijitambulisha kwa maofisa wa JWTZ, kuwa yeye ni ofisa wa jeshi hilo. Baada ya kujitambulisha alionyesha kitambulisho chake chenye namba D. 0595 kikiwa na jina la P. 15705 A.S Marco. Pamoja na utambulisho huo, maofisa wa jeshi walimtilia shaka luteni huyo  na kuamua kumkamata,” alisema Kamanda Njewike.

Aliongeza kwamba  polisi kwa ushirikiano na maofisa  hao, walifanya  upekuzi ndani ya gari la  mtuhumiwa aina ya Toyota Corola lenye namba za usajili T 289 AUF na kukuta vitu mbalimbali. “Katika upekuzi, tulifanikiwa kukuta picha za paspoti saizi tatu za mtuhumiwa, sare za JWTZ zenye cheo cha luteni na mihuri minne ya shule mbalimbali.  Mali zingine ni Sh 170,000 taslimu, cheti cha kuhitimu elimu ya sekondari kidato cha nne na cheti cha kuzaliwa cha Aloyce Zawadiel Solomoni,” alisema.

Alitaja vitu vingine kuwa ni vivuli vya vyeti vya elimu ya sekondari, cheti cha diploma, cheti cha udereva  na cheti cha elimu ya sekondari, mali ya Nelsoni John Ntandu, na kwamba katika upekuzi uliofanyika  chumba cha nyumba ya kulala wageni, Rock Side,  ya Majengo mjini Singida, walikamata Sh 500,000. Pamoja na hayo, alisema polisi wanaendelea na upelelezi zaidi na baada ya kukamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.