BINTI wa miaka 22, Ephrazia Maneno, mkazi wa Kijiji cha Nyaseke, Kata ya Bulela mjini Geita, anadaiwa kumuua kwa kumnyonga mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu kisha naye kujinyonga.
Tukio hilo limetokea Jumapili Agosti 18, 2019, saa saba mchana umbali wa mita 300 kutoka nyumba aliyokuwa akiishi ambapo alitumia khanga kujinyonga kwenye mwembe.
Maneno Kapunda, baba mzazi wa Ephrazia, amedai binti yake alikuwa akiishi na babu na bibi zake baada ya wazazi kutengana na hakueleza tatizo lolote kabla ya kufanya uamuzi wa kujiua.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyaseke, John Maguta, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba polisi walifika eneo la tukio na kuutoa mwili wa marehemu uliokuwa ukining’inia na kuruhusu familia kuendelea na taratibu za mazishi yaliyofanyika Jumatatu kijijini hapo.