
Taasisi ya Coconut (Coconut Foundation) ambayo ni asasi isiyo ya kiserikali kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na TAMISEMI imeaandaa mashindano ya kutamka herufi za maneno ya lugha ya Kiingereza, yenye maudhui ya kutia chachu kwa wanafunzi wa elimu ya msingi kujenga tabia ya kujisomea vitabu kwa wingi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika mkutano huo, Mtendaji wa Taasisi ya Coconut, Frank Mushi alisema lengo kuu la kuja na shindano hilo ni kumjengea mwanafunzi uwezo wa kujieleza na hivyo kugusa stadi muhimu za kimaisha katika kuwaandaa wawe nguvu kazi sahihi ya uchumi wa viwanda na biashara.
“Mashindano haya yanaendana sambamba kwa kuitikia wito wa Umoja wa mataifa (UN) kwenye mpango wa Malengo ya maendeleo endelevu (SDGs); lengo nambari 4 la ‘Elimu bora’
“Wanafunzi kutoka shule zaidi ya 100 wa mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na kwa mara ya kwanza Visiwa vya Zanzibar watachuana kuanzia ngazi ya shule mpaka ngazi ya kitaifa ambapo sasa mashindano haya yatafunguliwa rasmi Agosti, mwaka huu na kufikia kilele chake Novemba,” alisema Frank Mushi na kuongeza;
“Washindi 10 watakaopatikana wanatarajiwa kuwa mabalozi wa elimu ya usomaji wakitarajia pia kupata mialiko mbalimbali kuiwakilisha nchi katika ngazi ya kimataifa. Shindano hili litashirikisha shule za serikali na zile za binafsi, wadau wote wa elimu na umma kwa ujumla wake.”
Kwa mwaka 2019, mashindano haya yanaanzia ngazi ya shule ambapo washindi 10 hupatikana kufuzu ngazi ya kimkoa. Kutokana na uwingi wa shule, mkoa wa Dar es salaam kupitia manispaa za awali za kiutawala yaani Temeke, Ilala na Kinondoni zitafanya mashindano ya kimkoa hivyo kufanya mikoa 5 ukijumulisha Zanzibar na Lindi. Washindi 20 kutoka kila mkoa watafuzu mashindano ya kitaifa ili kupata washindi 10 bora kutoka makundi mawili kulingana na ngazi za madarasa.
Mwaka 2019 Coconut Foundation imeungwa mkono na mdhamini mkuu wa mwaka, Oxford University Press Tanzania Ltd.
Taasisi inazikaribisha shule mbalimbali kujisajili (Usajili wa Shule kushiriki utakoma rasmi tarehe 31 Agosti 2019), wadau mbalimbali wa maendeleo ya elimu wanakaribishwa kuunga mkono jitihada hizi na vijana waliohitimu elimu hasa katika fani za lugha wanakaribishwa kuomba nafasi ya kujitolea ili kukuza ueledi wao na nafasi za ajira.
Imeandaliwa na Neema Adrian/GPL