
UJENZI wa mradi wa bomba kubwa la kusafirishia mafuta kutoka Hoima nchini Uganda mpaka Bandari ya Tanga nchini Tanzania umesitishwa mpaka pale ambapo taarifa nyingine itatolewa.
Kwa mujibu wa mashirika ya habari ya kimataifa ya Reuters na Bloomberg yameeleza kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kampuni ya uchimbaji mafuta ya Tullow kushindwa kuwauzia Kampuni za Total ya Ufaransa na CNOOC ya China vitalu vya mafuta wiki iliyopita.
Kampuni ya Total ndiyo inasimamia ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,445 na tayari hatua za awali kuelekea ujenzi huo kama ramani, baadhi ya kandarasi na utanuzi wa bandari ya Tanga Tanzania zilishaanza.
“Shughuli zote za ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (East African Crude Oil Pipeline) ikiwemo kandarasi zimesitishwa mpaka hapo taarifa mpya itakapotolewa kutokana na kushindikana kwa mauzo ya visima,” ofisa mmoja nchini Uganda ameiambia Reuters kwa sharti la kutotajwa jina.
Makubaliano ya uuzwaji wa vitalu hivyo yalivunjika Agosti 29 kutokana na mzozo wa kodi na mamlaka za Uganda.
“Kuvunjika kwa makubaliano ya mauzo kunaleta sintofahamu juu ya nani atagharamia kitu gani katika kuendeleza mradi huo, ambao ungekuwa na mfumo sawia wa umiliki kama ule wa vitalu vya mafuta,” alisema ofisa huyo.
Uganda iligundua mafuta ghafi miaka 13 iliyopita, lakini uchimbaji wa kibiashara ulicheleweshwa kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu, ikiwemo bomba la mafuta. Mradi wa ujenzi wa bomba hilo ulipangiwa kugharimu dola bilioni 2.5, kutoka Hoima, Magharibi mwa Uganda mpaka Bahari ya Hindi, Bandari ya Tanga, Kaskazini mwa Tanzania.
Njia ya kupitisha bomba hilo ilikuwa ni moja ya masuala yaliyogonga vichwa vya viongozi wa Afrika Mashariki mwaka 2016. Awali ilitazamiwa bomba hilo lingepitia nchini Kenya na kuishia kwenye bandari ya Lamu, kabla ya serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutupa karata yake mezani.
Baada ya vishindo na vita ya chini kwa chini, Uganda iliamua kupitisha mafuta hayo nchini Tanzania. Kwa mujibu wa Bloomberg, kampuni ya Total imegoma kutoa kauli yeyote juu ya usitishwaji wa ujenzi.
CHANZO: BBC Swahili
Bloomberg ==> Total Suspends Planned $3.5 billion Uganda-Tanzania Oil Pipe
Reuters ===> Ugandan oil pipeline plan suspended due to collapse of Tullow-Total deal
Uganda Business News ===> Total E&P freezes work on Uganda-Tanzania oil pipeline