The House of Favourite Newspapers

Mauaji ya Akwilina… Mbowe, Wenzake Wana Kesi ya Kujibu – Video

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewakuta na kesi ya kujibu viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe,  katika kesi ya jinai namba 112/2018, inayowakabili yenye mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi.

Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Septemba 12, 2019,  na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba,  baada ya upande wa mashtaka kupitia Wakili Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi,  kuieleza mahakama hiyo kwamba imefunga ushahidi wake.

 

Baada ya Nchimbi kueleza hayo, Simba amesema mahakama hiyo imepitia vielelezo saba na ushahidi wa mashahidi wanane wa Jamhuri uliowasilishwa mahakamani hapo, na kujitosheleza kwamba washtakiwa wana kesi ya kujibu.

 

Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu-Taifa; John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara na Salumu Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu -Z’Bar.

Wengine ni Ester Matiko Mbunge wa Tarime Mjini; Halima Mdee, Mbunge wa Kawe; Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini; John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini na Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

 

Mbowe na wenzake wanatuhumiwa kufanya uchochezi wakati wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo katika jimbo la Kinondoni, kwenye viwanja vya Buibui na kisha kufanya maandamano.

 

Wanadaiwa kufanya maandamano hayo kupinga mawakala wao kutoapishwa kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo hilo. Tukio la maandamano hayo lilifanyika siku moja kabla ya siku ya uchaguzi huo Februari 16, 2018.

 

Jana katika kesi hiyo Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kipolisi Mbagala, Bernard Nyambari, alitoa ushahidi na kuieleza mahakama hiyo kuwa taarifa za kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline,  zinaonyesha alikufa akiwa hospitali ya Mwananyamala akipatiwa matibabu.

Alisema Akwilina alipata jeraha kichwani lililosababishwa na risasi, lakini hafahamu aliyempiga risasi mwanafunzi huyo. Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi tareje 17, 18 na 19 ambapo upande wa utetezi itaanza kuwasilisha utetezi wao.

 

View this post on Instagram

 

A post shared by Global Publishers (@globalpublishers) on

Comments are closed.