The House of Favourite Newspapers

Unachukua nafasi yako kama mke?

NI juma lingine tulivu kabisa tunakutana kwenye ukurasa huu ambao unapata fursa ya kusoma dondoo mbalimbali zinazoweza kuyaboresha maisha yako. Nikusihi tu uendelee kuwa mdau wa makala ninazoandika maana ni zenye manufaa kwenye maisha yako.  Mpenzi msomaji wangu, leo nitazungumzia mambo machache ambayo yanawahusu wanawake walio kwenye ndoa. Nawazungumzia wale ambao wameshindwa kuchukua nafasi zao kama wake za watu lakini na wale wenye kasumba ya kuigaiga mambo yasiyo na faida.

Hili la kuiga linawahusu wanawake wasio wajanja, wale malimbukeni ambao kamwe hawawezi kudumu kwenye ndoa zao. Katika hili la mke kuchukua nafasi yake nianze kwa kusema kwamba, wanawake wengi hujikuta wakisalitiwa au kuachwa kabisa na waume zao kutokana na ufahamu mdogo ama dharau ya mambo madogo.

Ni busara kutambua kuwa ndoa haina mambo madogo. Kila kitu kina umuhimu mkubwa kulingana na nafasi yake sambamba na utekelezaji wako. Mfano, kumpokea bahasha mumeo anaporejea kutoka kazini, huonesha unajali pamoja na kutimiza wajibu.

Mwanaume harogwi kwa limbwata ya sangoma, mahaba peke yake yanatosha. ‘Ukimhendo’ kwa kiwango kitakachomridhisha, hatowaza kukuacha. Unawezaje? Jibu ni rahisi, muoneshe unampenda na uthibitishe mapenzi yako kwa vitendo.

Daima hili liwe akilini mwako, mwanamke kupitia mapenzi yake ana uwezo mkubwa mno, lakini lazima awe anajua kutimiza wajibu wake kwenye uhusiano. Kama mpenzi wako anakuacha, ujue kuwa kuna mambo unayomkosea na kuyafanya mapenzi yako yageuke kuwa kero kwake.

Unyenyekevu kwa wanawake wa kisasa kimekuwa ni kitu adimu, kiasi ambacho kimekuwa kikihatarisha uhusiano wa watu wengi. Wanaume wanawapenda wanawake ambao hujionesha waziwazi kuwa wenyewe ni wasaidizi wao wakuu katika masuala mbalimbali. Anza leo kutimiza wajibu wako.

Lakini pia kaa ukijua kwamba, wanaume wengi wanajiona waliokamilika endapo watakuwa wameoa wake wajanja. Sababu ya wanaume kuwapenda wanawake wajanja ni kukwepa aibu wanazoweza kuzipata pindi watakapokuwa kwenye uhusiano na washamba. Huogopa kujiingiza katika mapenzi na watu wasiokuwa na uelewa mpana wa mambo ambao kutokana na tongotongo za ufahamu, hujikuta wakiwa mafundi wa kuiga mambo ya kileo tena ya hatari.

Washamba mara nyingi huwa ni malimbukeni, hujifunza mambo yasiyokuwa na faida kwa imani kwamba naye ataonekana mtu kati ya watu. Wanawake wa aina hii ni rahisi kuwaingiza wenzi wao katika hasara kubwa. Hawakawii kuiba, ni rahisi kuharibu vitu, wao ni wabadhirifu na wanapenda makuu!

Wanawake malimbukeni huharibika katika vikao vya ususi, kutokana na sifa kubwa ya umbeya kwenye sehemu hizo. Wanaume wasiokuwa na subira hujikuta wakiwapiga teke wenzi wao mapema, mara tu wanapoanza kuhisi nyendo zisizoeleweka kwa vipenzi vyao.

Tumekuwa tukishuhudia wanawake malimbukeni wakiiga tabia za ulevi wa pombe au mihadarati kutoka kwa marafiki zao. Wakibadilika na kuwa wafuska kupindukia, huku wakiwapanga mabwana kila kona. Si wameshauriwa mwanamke mafiga matatu? Ndiyo anatekeleza kwa vitendo!

Mwanamke mjanja hawezi kuiga hovyo hovyo, siku zote anajua kitu cha kuanzia na kinachofuata. Hawadanganyiki kwa penzi la pesa, wanaelewa malipo yake ni makubwa. Wakichombezwa kuhusu mabuzi wao ni wajuvi, kwa hiyo hudharau na kushika hamsini zao. Ndiyo maana wanaume wanawapenda!

Nafasi ni finyu, niishie hapo kwa leo.

Comments are closed.